Friday, January 5, 2018

Viwanda vya samaki vyashushiwa rungu


WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI, LUHAGA MPINA.

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, amewaamuru wamiliki wa viwanda vitano vya kuchakata minofu ya samaki vilivyoko jijini Mwanza kulipa faini ya Sh. milioni 180 ndani ya saa 24, baada ya kubainika kupokea na kuchakata samaki wasioruhusiwa.

Kwa kufanya hivyo, alisema wamekiuka  Sheria ya Uvuvi namba 22 ya mwaka 2003 na kanuni zake za mwaka 2009  sambamba na Sheria ya usimamizi wa Mazingira namba 20 ya mwaka 2004.

Pia Waziri Mpina amechukizwa na kitendo cha viwanda hivyo kufadhili uvuvi haramu na kueleza kuwa ni bora kutokuwa na kiwanda hata kimoja cha samaki kuliko kuendelea kuwa na viwanda vinavyofadhili uvuvi haramu na kutishia kuvifunga viwanda vyote sambamba na kutaifisha samaki, magari na boti zinazobeba samaki wasioruhusiwa.

Waziri Mpina alisema hayo jana kwa nyakati tofauti alipofanya ziara kutembelea viwanda vinavyochakata samaki jijini Mwanza ambapo pia alimuagiza Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk.  Yohana Budeba, kuwasimamisha kazi maofisa watatu wa Kitengo cha Udhibiti wa usalama na ubora wa mazao ya uvuvi kituo cha Mwanza kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria na kulisababishia taifa hasara kubwa.

Maofisa hao ambao Waziri Mpina aliagiza wasimamishwe kazi na kuchukuliwa hatua kali za kinidhamu ni Philemon Mugabo, Dorina Mlenge na John Bosco Rubajuna.

“Haiwezekani mimi nije hapa kukagua samaki waliovuliwa na watendaji wa Serikali ngazi zote wapo na sijawahi kupata taarifa yoyote wizarani ya hatua zilizochukuliwa iwe kwa kupigwa faini au laa hivyo watumishi wa Serikali wote wanaohusika na Kitengo cha udhibiti wa usalama na ubora wa mazao ya uvuvi kituo cha Mwanza wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi wasimamishwe kazi kuanzia leo (jana) na wachukuliwe hatua kali za kinidhamu,’’  aliagiza Mpina.

Waziri Mpina alitaja viwanda  vilivyokutwa vikichakata samaki wasioruhusiwa wakiwamo samaki wazazi na wachanga  na idadi ya kilo zilizokamatwa kwenye mabano ni Nile Perch Fish (920), Victoria Fish (131), Nature Fish (150), Omega Fish (580) na Tanzania Fish Processing (842).

Magari ni 41, boti 15, nyavu haramu 294 wakiwa na samaki wachanga na wazazi ambapo sheria inakataza kuvuliwa samaki chini sentimita  50 na juu ya sentimita 85.

Majina ya viwanda hivyo na faini zao walizotozwa Nile Perch Sh. milioni 25, Tanzania Fish Processing  Sh. milioni 50, Victoria Perch Sh. milioni 30, Nature Fish Sh. milioni 25 na Omega fish Ltd Sh. milioni 50.

Alisisitiza adhabu hiyo ni ya kwanza na ya mwisho na ikithibika tena wenye viwanda waendelea kufadhili uvuvi haramu hatua za kuvifunga viwanda na kutaifisha mali ikiwamo mitumbwi, boti na magari yatakayokuwa yanabeba samaki hao itafuata.

Mpina alisema ukanda wa Ziwa Victoria ulikuwa na viwanda 13 vya kuchakata samaki vilivyokuwa na uwezo wa kuchakata tani 1,065 kwa siku, lakini kutokana na kushamiri kwa uvuvi usiongatia sheria kumesababisha viwanda 5 kufa kutokana na kukosekana malighafi na viwanda 8 vilivyobaki sasa vinachakata tani 171 tu kwa siku huku ajira zikiwa zimeporomoka kutoka 4, 088 na kufikia 2,179.

Mpina alisema Rais John Magufuli alishatoa maagizo kwa wavuvi kuachana na uvuvi haramu sambamba na wenye viwanda kutofadhili uvuvi huo huku pia Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan naye akisisitiza jambo hilo na Wizara ya Mifugo na Uvuvi ikikemea vikali huku Sheria za nchi nazo zikikataza  jambo hilo, lakini wenye viwanda kwa makusudi wameamua kudharau maagizo hayo, jambo ambalo Wizara ya Mifugo na Uvuvi haliwezi kukubalika kamwe.

Alivitaka viwanda kuwa chimbuko na chemchem ya kupinga uvuvi haramu kwa kutokubali kupokea samaki waliovuliwa kinyume cha sheria wakiwamo samaki wazazi na samaki wachanga na kuwataka kutoa taarifa haraka kwenye vyombo vya dola pindi wanapoletewa samaki wa aina hiyo.


No comments:

Post a Comment