Friday, January 5, 2018

Wajumbe wa CCM wamsaka diwani wake aliyesababisha wao kushindwa Uchaguzi


Dar es Salaam. Wajumbe wa CCM wanaoingia kwenye Baraza la Madiwani la Jiji la Dar es Salaam, wamesema wapo katika hatua za mwisho za kumpata mjumbe mwenzao aliyesababisha wao kushindwa uchaguzi wa naibu meya wa jiji hilo.

Uchaguzi huo uliokuwa na mchuano mkali kutokana na kila upande kuwa na wajumbe kumi na moja, ulifanyika juzi katika ukumbi wa Karimjee na Mussa Kafana wa CUF akiungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) aliibuka kidedea kwa kupata kura 12 dhidi ya 10 alizopata Mariam Lulida wa CCM.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, mjumbe baraza hilo CCM, Abdallah Chaurembo alisema tayari wanao ushahidi na wameshaanza kumbaini mjumbe ambaye alisababisha chama chao kushindwa katika uchaguzi huo.

“Tunataka kuirahisishia kazi kamati ya siasa ya mkoa kwa kumpata kwanza mjumbe huyu, halafu wao ndiyo watakaokuwa na jukumu la kumtangaza na kumchukulia anazostahili kwa mujibu wa makosa yake,” alisema Chaurembo.

Chaurembo ambaye pia ni Meya wa Temeke alisema walishaanza kumbaini mjumbe huyo kabla ya kazi ya kuhesabu halijakamilika na kudai kwamba hakuwa na nia ya dhati na CCM.

“Tulishakijua alichokuwa akikifanya, kwanza alikuwa anatetemeka wakati anaenda kupiga kura. Wakati yupo katika eneo la kupiga yeye ndiyo alitumia takriban dakika tano wakati wenzake nusu dakika.

“Hivi mtu unachukua takriban dakika tano nzima katika kupiga kura, una nini wewe, ina maana hujui kusoma wala kuandika? Alihoji Chaurembo. Nawaambia WanaCCM tutampata mtu huyo very soon (muda mfupi).

Alisema wameamua kushughulikia jambo hilo, ili iwe funzo kwa madiwani wengine wasiokitakia mema chama hicho na kwamba, hiyo itakuwa njia ya kuwaondoa wale viongozi wasio na masilahi na CCM.

Alieleza kuwa wajumbe wa CCM katika baraza hilo, wana imani wameshindwa katika uchaguzi kwa hoja mbili ambazo ni Ukawa kutumia utemi wakati kura mbili ziliharibika, na mjumbe mwenzao kuharibu kura na siyo kumpigia kura mgombea wa upinzani.

Katika uchaguzi huo, Chaurembo na meya mwenzake wa Ubungo (Chadema), Boniface Jacob nusura wazichape wakati wa shughuli ya kuhesabu kura kama si wajumbe wa uchaguzi huo kuwatenganisha.

Chaurembo aliendelea kwa kufafanua kuwa mjumbe huyo akishapatikana wajumbe wa CCM wa baraza ndiyo watakaokuwa mashahidi kwenye kamati ya siasa ya mkoa.

Naibu Meya asimulia alivyobebwa

Wakati Chaurembo akieleza hayo, naibu meya mteule, Kafana ameeleza namna alivyochukuliwa nyumbani kwake na kupelekwa kupiga kura akiwa mgonjwa.

Kafana alimweleza mwandishi wetu jana kwamba alikuwa katika hali mbaya kiafya kwa kuwa alikuwa akisumbuliwa na malaria, kifua na tumbo la kuhara.

Alisema baada ya kuwa na hali hiyo, alitoa taarifa kwa ofisi ya mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, ambayo iliamuru kutuma mwakilishi kwa ajili ya kuthibitisha kama anaumwa.

“Alikuja mwakilishi kutoka ofisi ya mkurugenzi ambaye alikwenda hadi katika zahanati niliyokuwa nikitibiwa na kupata uthibitisho, kisha akaja nyumbani kwa kupiga picha vyeti na kuniona,” alisema Kafana.

Alisema akiwa amepumzika baada ya kutoka hospitali, kadri muda ulivyokwenda simu zilikuwa zikipigwa kwa ndugu zake zikieleza kuwa anatakiwa kwenda kupiga kura hata kama ni mgonjwa na kwamba uchaguzi hauwezi kuahirishwa.

“Waliwapigia ndugu zangu kwamba wanakuja kunichukua na wakahakikishia nisiwe na wasiwasi kila kitu kitakwenda sawa. Haukupita muda alikuja Kubenea (Saed –Mbunge wa Ubungo) na vijana wengine kunichukua mkukuku.

“Ule mwendo haukuwa wa kawaida, gari lilikimbia sana kuhakikisha nashiriki uchaguzi. Ingekuwa jambo hili ni la mgombea binafsi nisingeenda kwa sababu nilikuwa najisikia vibaya, lakini wajumbe wenzangu wa Ukawa wakasema haiwezekani lazima nishiriki hata kama mgonjwa,” alisema Kafana.

Hata hivyo, baada ya kuingia katika ukumbi wa mikutano Kafana hakuweza kupiga kura badala yake alisaidiwa na Kubenea ambaye alikuwa kiongozi kwa upande wa wajumbe wa Ukawa.

Kafana alisema alikuwa na uhakika wa kuibuka kidedea kutokana na idadi ya namba za wajumbe wanaounda Ukawa, lakini kutokana wajumbe wenzake kumhitaji ilimlazimu kuitikia wito huo huku akiwa taabani.

“Nilikuwa najiamini katika uchaguzi ule kutokana na uhusiano mzuri uliopo kati yangu na wajumbe wa Ukawa na CCM. Ndiyo maana sikushangaa kusikia kupigiwa kura na mmoja wajumbe kutoka CCM,” alisema Kafana.

Kuhusu madai ya yeye kuigiza mgonjwa wakati ni mzima wa afya, Kafana alisema “ Mimi ndiyo mgonjwa, nawashangaa hao wanaosema mimi ni mzima. Isingekuwa wajumbe wa Ukawa kunitaka niende, binafsi nisingeshiriki. Kwenda na hali ile ni kujidhalilisha.”

Kafana aliwashukuru wajumbe wenzake kwa kumuwezesha kutetea nafasi hiyo na kwamba akisema wamefanya kazi kubwa.

Alisema awali, alijua kwamba uchaguzi huo ungekuwa wa kawaida lakini kwa hali ilivyokuwa, dhana hiyo ilikuwa ni kinyume chake.


No comments:

Post a Comment