Saturday, January 13, 2018

THE GRAVES OF THE INNOCENTS (MAKABURI YA WASIO NA HATIA)- 54


ILIPOISHIA:
Ni kweli nilikuwa na marafiki wengi wanaonipenda kule nyumbani Chunya lakini sikuwa tayari hata kidogo kuona mtu yeyote asiye na hatia anapatwa na matatizo kwa sababu yangu. Nilijikuta nikijilaumu sana kwa upumbavu wangu wa kutaka kwenda kujionea mwenyewe kilichotokea kule Mlandizi.
“Tunasubiri jibu lako,” baba alinizindua kutoka kwenye lindi la mawazo.
SASA ENDELEA…
“Lakini baba…”
“Lakini nini? Hakuna mjadala, kinachotakiwa hapa ni utekelezaji tu,” alisema baba na kunitishia kwamba endapo sitatoa majibu, kwa kuwa yeye anawafahamu marafiki zangu, atapendekeza jina lolote.
Kwa mara nyingine nilikuwa nimeingia kwenye mtego hatari wa kutaka kupoteza maisha ya mtu asiye na hatia kwa sababu ya uzembe wangu. Nilijisikia vibaya sana, nikashindwa kuzuia machozi yasiulowanishe uso wangu.
“Hata sisi mwanzo tulikuwa kama wewe, utazoea tu,” alisema baba yake Rahma. Sikujua ni nini hasa kilichotokea kwenye akili za baba na baba yake Rahma mpaka wachukulie kitendo cha kukatisha maisha ya mtu asiye na hatia kuwa cha kawaida kiasi kile.
Baada ya kulumbana kwa muda mrefu, baadaye niliamua kusalimu amri, nikamtaja rafiki yangu kipenzi, Sadoki. Kilichosababisha nikamchagua Sadoki, ni kwa sababu dakika za mwisho, urafiki wetu ulikuwa umeingia dosari baada ya siku moja kumkuta akishirikiana na watu wengine kumteta baba yangu kwamba alikuwa mchawi.
Kwa kipindi hicho, nilikuwa bado sijajua ukweli kwamba baba ni mchawi au mganga kwa sababu mara zote nilizokuwa namuuliza alikuwa akisema kwamba yeye ni mganga na wala si kweli kwamba anajihusisha na mambo ya kishirikina kwa hiyo yeyote niliyemsikia akizungumza mabaya ya baba, alikuwa akigeuka na kuwa adui yangu.
Siku nyingi zilikuwa zimepita tangu siku tulipotaka ‘kuzichapa’ maana baada ya kumkuta akimsema vibaya baba, nilimjia juu sana, kama isingekuwa watu wazima waliokuwa jirani nasi, huenda tungepigana na kuumizana sana.
Hata hivyo, tukio hilo moja halikuharibu ukweli kwamba tulikuwa marafiki wakubwa kwa sababu nakumbuka mara kwa mara alikuwa akija kwetu, na mimi nilikuwa nikienda kwao. Kwa kifupi ni kwamba ukiachilia mbali hiyo dosari ndogo iliyotokea, tulikuwa tumeshibana kisawasawa.
Baada ya kumtaja jina, sikuweza kuendelea kukaa mle chumbani, nilitoka na kwenda bafuni huku nikichechemea, nikajifungia na kuanza kulia kwa uchungu, baba na baba yake Rahma wakabaki chumbani kwangu wakiendelea kujadiliana mambo yao. Nililia mpaka macho yakawa mekundu kabisa, nilimuonea huruma Sadoki, nilimuonea huruma mama yake na wadogo zake.
Walikuwa wakimtegemea kwa sababu baba yao alifariki wakiwa bado wadogo kwa hiyo baada tu ya kumaliza shule ya msingi, Sadoki alikuwa akienda kufanya vibarua kwenye machimbo ya dhahabu na fedha kidogo alizokuwa akizipata ndizo zilizokuwa zikiihudumia familia yao.
Nikiwa bado naendelea kulia kule bafuni, baba alikuja kunigongea, ikabidi ninawe uso harakaharaka, nikatoka huku uso wangu nikiwa nimeuinamisha. Tulirudi chumbani kisha akaanza kunipa maelekezo kwamba usiku wa siku hiyo tunatakiwa kusafiri kuelekea Chunya.
“Tukifika, inabidi twende mpaka nyumbani kwa huyo rafiki yako, kuna dawa utaitega mlangoni, asubuhi akiwa anatoka anatakiwa airuke, akishairuka tu kazi itakuwa imekwisha.
“Sasa tutaendaje Chunya na kufanya hivyo unavyosema kabla hakujapambazuka?” niliuliza kwa sababu kama ni mabasi, muda huo tusingeweza kupata la kwenda Mbeya na hata kama lingepatikana, tusingewahi kama baba alivyokuwa anasema.
“Hutakiwi kuhoji sana, sikiliza kwa makini ninachokueleza,” baba alinikatisha, akaendelea kunipa maelezo ya namna ya kukamilisha zoezi hilo ambayo kwangu yalikuwa yakiingilia sikio la kushoto na kutokea la kulia.
Sikuona sababu yoyote ya kumuadhibu Sadoki kwa makosa ambayo nilikuwa nimeyafanya mwenyewe, nikajikuta nikijihisi hatia kubwa mno ndani ya moyo wangu. Basi tuliendelea kuzungumza pale, kisha baba akaniambia nijiandae kwa safari.
Walitoka na kuniacha nimejilaza kitandani, machozi yakaanza kunitoka tena na kwa sababu nilikuwa nimejilaza kwa kutazama juu, yalikuwa yakichuruzika kupitia kona za macho yangu mpaka kichwani na kupotelea kwenye shuka lililokuwa limetandikwa pale kitandani.
“Hivi ndiyo nimeshakuwa mchawi?” nilijiuliza swali kama mwendawazimu. Ni mimi ndiye niliyekuwa na shauku kubwa ya kuwa na nguvu zile za ajabu lakini sijui ni kutoelewa au ni kitu gani, ndani ya muda mfupi tu nilishaanza kuhisi kwamba pengine nimebeba mzigo mzito ambao sina uwezo nao. Zile kauli za baba akinikebehi kwamba bado nina akili za kitoto zikawa zinajirudia ndani ya kichwa changu.
Niliendelea kutafakari kwa kina na baadaye usingizi mzito ulinipitia, nikiwa usingizini nilianza kuota ndoto za ajabuajabu na kusababisha niwe nashtuka mara kwa mara. Baadaye ndoto hizo zisizoeleweka zilikoma, nikalala mpaka majira ya saa mbili za usiku nilipokuja kuzinduliwa na sauti ya baba aliyekuwa akiniita, nikakurupuka na kuamka.
“Umeshajiandaa?”
“Ndiyo,” nilimjibu huku nikijifikicha macho na kujinyoosha. Ukweli ni kwamba sikuwa nimejiandaa chochote.
“Haya nifuate.”
“Lakini bado sijala.”
“Utaenda kula mbele ya safari,” alisema baba huku akinihimiza nisimame. Nilishuka kitandani, miguu ikawa inauma sana hasa kwenye nyayo kutokana na majeraha ya ile miiba niliyotolewa na Rahma. Ilibidi nijikaze kisabuni kwa sababu ni mambo ambayo nilijitakia.
Tulitoka mpaka nje bila kuonekana na mtu yeyote, tukamkuta baba yake Rahma amesimama mlangoni, akionesha kwamba alikuwa akitusubiri. Alinipa kofia kubwa na kuniambia niivae, sikumuelewa kwa sababu gani amefanya vile. Tulitoka, mimi nikiwa katikati na kwenda hadi pale kwenye maegesho ya Bajaj, tukaingia kwenye mojawapo na baba yake Rahma akampa maelekezo dereva kwamba atupeleke Mwenge.
Sikuwa napajua Mwenge zaidi ya kupasikia tu, ni hapo ndipo nilipoelewa kwa nini baba yake Rahma alinipa ile kofia kwa sababu japokuwa nilikuwa nimeivaa, na kuziba sehemu kubwa ya uso wake, wale madereva Bajaj walikuwa wakinitazama kama wanaotaka kuhakikisha kama ni mimi kweli au laah!
Sikuwajali zaidi ya kuwadharau kwa sababu sasa nilikuwa na uwezo wa kumfanya mtu yeyote ninavyotaka mimi. Bajaj ilianza kukata mitaa na baada ya muda, tuliingia kwenye barabara ya lami iliyokuwa na magari mengi.
Safari ikaendelea mpaka tulipofika mahali kwenye mataa yenye mwanga mkali ambayo licha ya kwamba ilikuwa ni usiku, yalikuwa yakiangaza sehemu yote, watu wakiendelea na shughuli zao utafikiri ni mchana.
Tulishuka kwenye Bajaj huku nikishangaa huku na kule, moyoni nikawa najisemea ‘mjini kuzuri sana’. Tukaanza kuvuka barabara mbili pana ambazo katikati zimetenganishwa na bustani ya maua.
Kiukweli kama ningekuwa peke yangu, nisingeweza kuvuka kwa sababu kulikuwa na magari mengi mno, nikawa naung’ang’ania mkono wa baba Rahma maana baba naye alionesha kuwa na mchecheto.
Tulivuka salama mpaka upande wa pili ambako tulipanda magari mengine yanayoelekea Kunduchi. Kila kitu kilikuwa kigeni kwangu, safari ikaanza mpaka tulipofika Kunduchi, tukashuka kwenye gari na kuanza kutembea kwa miguu. Sikuwa najua tunaelekea wapi, baada ya muda tukatokezea kwenye makaburi yaliyokuwa karibu na bahari.
“Haya ni makaburi ya Wagiriki, ni ya zamani sana na hapa ndiyo hutumika kama njia ya kuingia na kutoka kwenda sehemu yoyote,” baba yake Rahma alinielekeza kwa sauti ya upole, tukaingia mpaka katikati kabisa ya makaburi hayo, mahali palipokuwa na mti mkubwa wa mbuyu.
“Tunaenda Chunya, hutakiwi kwenda kinyume na maelekezo tunayokupa, ukifanya uzembe tu, kitakachokutokea ni juu yako,” alisema baba kwa sauti ya msisitizo, nikawa natingisha kichwa kukubaliana naye. Tulikaa chini na kuweka kama duara hivi, tukashikana mikono kisha nikaambiwa nifumbe macho.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue au bofya Simulizi za Majonzi kusoma mwendelezo.


No comments:

Post a Comment