“OH My God! It is a ruptured pregnancy!”(Mungu wangu! Kumbe mfuko wa uzazi umepasuka!) aliongea kwa sauti Dk. Namshitu Fundikira, bingwa wa upasuaji wa matatizo ya wanawake .
“Kweli?” Daktari mwingine aliyekuwa karibu aliuliza.
“Kabisa, tunachohitaji kufanya hivi sasa ni kumkimbiza haraka sana chumba cha upasuaji ili tujaribu kuokoa maisha ya mama na mtoto, tukizidi kuchelewa tutapoteza wote wawili au mmoja wao.”
Yalikuwa ni maongezi ya kundi la madaktari ndani ya chumba cha wagonjwa mahututi katika hospitali ya Good Samaritan iliyopo eneo la Mwenge jijini Dar es Salaam, mwanamke alikuwa amelala kitandani, ujauzito wake ukionekana bayana, mtu mwenye akili timamu hakuhitaji shahada yoyote kuelewa ukali wa maumivu aliyokuwa nayo, jasho jingi lilikuwa likimtoka na kulowanisha mashuka huku akitupa miguu yake huku na kule.
“Ana CPD!” Dk. Fundikira alitamka maneno hayo akimaanisha Cephalo-Pelvic- Disproportion, yaani hapakuwa na uwiano kati ya kichwa cha mtoto na nyonga ya mama, pengine mtoto alikuwa mkubwa na nyonga ndogo hivyo alikuwa ameshindwa kutoka nje kwa njia ya kawaida, akapasua mfuko wa uzazi.
Maisha ya mama yalikuwa katika hatari, hapakuwa na muda wa kupoteza kama kweli nia ya kuokoa maisha ilikuwepo. Madaktari walikimbia haraka chumba cha upasuaji kumsubiri mgonjwa, ambaye dakika kumi tu baadaye aliingizwa, timu yote ya watu wasiopungua kumi ikaingia kazini.
“Unaitwa nani?” Dk. Pascal Rwezaura, bingwa wa dawa za usingizi alimuuliza mgonjwa wakati akimchoma sindano kwenye mshipa.
“Jackline!”
“Jackline nani?”
“Manyilizu.”
“Mume wako yuko wapi?”
“Sina mu…” hakuweza kujibu swali hilo hadi mwisho, akaingia usingizini na upasuaji ukaanza dakika tano baadaye kila kitu kilipokuwa tayari, Dk. Fundikira, binti wa miaka ishirini na sita, mwenye elimu ya kutosha juu ya upasuaji aliongoza jopo la madaktari kuokoa maisha ya mgonjwa na mtoto.
Upasuaji ulifanyika kwa saa nne, ndipo taarifa zikapatikana kuwa mama na mtoto wake wote walikuwa wamenusurika kifo, ingawa mfuko wa uzazi uliondolewa, hiyo ilimaanisha mwanamke huyo asingepata mtoto tena maishani.
“Hongera sana daktari!” muuguzi alimwambia Dk. Fundikira.
“Nakushukuru sana Diana, muujiza umetokea, mtoto ni mzima kabisa wala hajaumia sehemu yoyote, nilikuwa na wasiwasi kwamba ubongo wake kuwa umeathirika lakini la! Ana afya njema mno, nasikitika tumelazimika kuuondoa mfuko wa uzazi kwani umepasuka vibaya mno!”
“Kwani kulitokea nini?”
“Ninahisi huko alikotokea, walimchoma sindano ya Oxytocin, kwa lengo la kumwongezea uchungu bila kufahamu kuwa mtoto alikuwa ameshindwa kupita kwenye nyonga ndogo, mfuko ukapasuka!”
“Uzembe wa hali ya juu!”
“Sana!”
***
Saa sita baadaye Jackline Manyilizu akiwa wodini alizinduka usingizini, mtoto alikuwa kando yake, machozi ya furaha yakamtoka. hakuamini alichokishuhudia kwa macho yake, kwamba ni yeye aliyekuwa amezaa mtoto mzuri kiasi hicho.
Mtoto alikuwa mchanganyiko wa Mwafrika na Mzungu, kwa kasi taswira za baba wa mtoto zikamwijia akilini na maonyo yote aliyopewa kwamba kamwe asifungue mdomo wake kusema chochote, akambusu mwanaye kwenye paji la uso.
“Nitamwita mwanangu Theresia!” aliongea akijifuta machozi.
***
Nyumba ya Jackline Manyilizu ilikuwa jirani kabisa na Parokia ya Mwenge ya Kanisa la Redemption Church Of God, ambalo watu wengi waliufananisha mfumo wake wa utendaji kama Kanisa Katoliki, tangu kuanzishwa kwake na watu waliojitenga na Kanisa Katoliki miaka ya sitini dhehebu hilo lilikuwa limekua na kujipatia wafuasi wengi sana nchini Tanzania.
Lilikuwa na Askofu mkuu, mapadri, watawa, makatekista kama tu ilivyokuwa kwa Kanisa Katoliki, tofauti pekee ambayo dhehebu hili lilikuwa nayo na Kanisa Katoliki ni namna ya kuendesha ibada, ndani ya Redemption Church ibada iliendeshwa Kilokole zaidi, watu wakiimba mapambio na kurukaruka wakimsifu Mungu jambo ambalo ndani ya Kanisa Katoliki halikufanyika.
Kwa sababu ya umasikini mkubwa, Jackline, alikuwa mwanamke mrembo lakini mchafu na aliajiriwa na Parokia hiyo kama mfagizi na mpishi wa mapadri, kazi aliyoifanya kwa miaka mingi kwa uaminifu mkubwa, akapumzika tu alipopatwa na ujauzito.
Aliporuhusiwa kutoka hospitali alirejea kwenye kibanda chake kidogo akiwa na mtoto wake, wafanyakazi wenzake ndiyo walimsaidia kumtunza mpaka alipopata nguvu za kujisimamia mwenyewe, hakutaka watu wengi sana wafike nyumbani kumwona mtoto wake, rangi ya Theresia ingeweza kuzua maswali mengi ambayo hakuwa tayari kuyajibu.
Miezi mitatu baadaye akiwa amemleta mtoto wa shangazi yake kutoka kijijini kwao Msowelo, wilayani Kilosa, aliamua kurejea kazini, wiki moja tu baadaye Padri Antonio Slivanio, alirejeshwa na shirika lake nchini kwao Ufaransa, sababu haikueleweka na wengi lakini Jackline alielewa kilichokuwa kikiendelea.
“Never open ya maut’ and say anything’” Maneno hayo ya Padri Antonio yaliendelea kuzunguka kichwani mwake.
Theresia alikuwa mtoto mrembo mno, mchanganyiko wake wa mama Mtanzania na baba Mzungu ulitia ganzi akili za watu wengi kila walipomwona, haikuwa rahisi hata kidogo kuamini mtoto huyo alikuwa wa Jackline.
Kwenye umri wa miaka miwili na nusu, Theresia alilazimika kupelekwa shule ya awali iliyokuwepo hapo hapo parokiani, haikuwezekana tena kuendelea kumficha mtoto ndani, jina aliloanzishwa nalo shule ni la Theresia Manyilizu, wengi walijiuliza maswali mengi bila kupata majibu juu ya baba wa mtoto.
“Magari yatagongana nyumbani kwao, kweli Tanzania tumebarikiwa kuwa na wanawake warembo lakini sijawahi kuona mtoto mzuri kama huyu, ona pua yake utafikiri Mtusi, shingo utadhani Muethiopia, midomo utafikiri Msudani, masikio utafikiri Msomali, kidevu utafikiri Msukuma! Huyu mtoto mrembo wacha mchezo bwana!” dereva mmoja wa Parokia alisikika akititirika maneno bila kituo huku wenzake wakimsikiliza.
Theresia aliendelea kukua kwa kimo na akili, uwezo wake shuleni ulikuwa mkubwa mno, kuanzia chekechea akisomeshwa na Kanisa mpaka darasa la saba hakuwahi kupata alama B kwenye masomo yake, hivyo ndivyo ilivyokuwa hata alipokuwa Sekondari ya St. Columbus ambayo pia ilimilikiwa na Shirika la Redemption Missionaries lililokuwa chini ya kanisa.
“Nataka uwe daktari mwanangu!”
“Lakini mimi nisingependa kuwa daktari!”
“Kwa nini?”
“Nataka kuwa mtawa!”
“Acha utani wako, mtawa? Unayafahamu maisha ya watawa mwanangu? Uwe mtawa nisipate mjukuu? Nani atanitunza? Wewe ndiye tegemeo langu mwanangu!”
“Nataka kuwa mtawa mama, huko ndiko moyo wangu ulikoelekea, nimtumikie Mungu!”
“Mtawa mwenye uzuri huu? Theresia, umekuwaje?”
“Kwani ukiwa mrembo huwezi kuwa mtawa mama? Urembo huu aliyenipa ni Mungu, nitamrudishia yeye kama alivyonipa, sitaki wanaume maishani mwangu, mateso uliyoyapitia wewe nisingependa kukutana nayo mimi, hivyo basi hakuna kingine ninachokihitaji zaidi ya utawa!”
“Haitawezekana!” mama alimaliza mjadala huo.
Matokeo ya mtihani wa kidato cha nne yalipotoka, Theresia alikuwa amepata daraja la kwanza, pointi 7, akiongoza Tanzania nzima, wanafunzi huwaita waliofaulu kama yeye kwa jina la Tanzania One, akaalikwa ikulu pamoja na walimu wa shule yake na wanafunzi wengine tisa waliokuwa kwenye orodha ya kumi bora.
Aliyeshika namba mbili alikuwa ni Joshua James, kutoka Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Umbwe iliyoko Kilimanjaro, waliongea mengi sana na Theresia baada ya kukabidhiwa zawadi zao, kijana huyo akamwambia yeye alitaka kuwa daktari bingwa wa wanawake ili aokoe maisha ya akina mama.
“Wewe?”
“Nataka kuwa mtawa.”
“Mtawa?”
“Ndiyo.”
“With that brain?”(na akili yote hiyo?)
“Kwani watawa hawatakiwi kuwa na akili nyingi?”
“Mh!”
“Nitampa Mungu zawadi ya akili alizonipa.”
“Kwa hiyo huna mpango wa kuolewa?”
“Kabisa, sitaki kuujua utupu wa mwanaume mpaka naingia kaburini.”
“Na uzuri wote huo?”
“Huo ndiyo uamuzi na dhamira yangu…”
Je, nini kitaendelea katika hadithi hii? Fuatilia Jumapili ijayo katika gazeti la Spoti- Xtra! Nakuhakikishia hautajuta kuisoma hadi mwisho.
Na Shigongo Eric
No comments:
Post a Comment