Friday, January 5, 2018

Wahukumiwa kwenda jela kwa unyang'anyi wa silaha


Unyang’anyi wa silaha wamtupa jela Rais Sinza

WATU watano akiwamo mfanyabiashara Morris Malianga maarufu kama rais wa Sinza na wenzake wanne wamehukumiwa kwenda jela miaka 150 baada ya kupatikana na hatia ya unyang’anyi wa kutumia silaha.

Mbali ya Rais wa Sinza, wengine waliohukumiwa ni Flano Masulu (Singu), Jeremiah Mgori, Sandru Kamugisha na Sadick Bwanga.

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, baada kupitia ushahidi wa mashahidi wa Jamhuri kuthibitisha makosa dhidi yao katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.

Alisema bila kuacha shaka mahakama yake imeridhika na ushahidi wa upande wa Jamhuri umethibitisha makosa dhidi yao.

“Mahakama yangu inawatia hatiani washtakiwa wote watano kila mmoja atakwenda jela kutumikia kifungo cha miaka 30...adhabu hii naitoa kwa mujibu wa sheria kwamba mtuhumiwa anapokutwa na hatia katika makosa ya unya’ng'anyi mahakama inawahukumu kifungo hicho,” alisema Hakimu Mashauri.

Kabla ya hukumu hiyo, wakili wa utetezi, Nehemiah Nkoko, aliiomba mahakama kuwapunguziwa adhabu kwa kuwa ni wakosaji wa mara ya kwanza na wameshakaa mahabusu miaka miwili.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanadaiwa Desemba 22, 2015 maeneo ya Mabibo Luhanga, washtakiwa waliiba Dola za Marekani 8,600 (Sh. milioni 18 kwa wakati huo).

Shtaka jingine wanadaiwa kuwa waliiba tena Sh. 2,500,000, kompyuta mpakato, simu nne vyote vikiwa ni mali za Anderson Balongo.

Baada na kabla ya wizi huo, washtakiwa waliwatishia kwa bastola Zeno Mriwa, Aneth  Paulo na  John Mkundi ili kujipatia fedha hizo.



No comments:

Post a Comment