Friday, January 5, 2018
Breaking News: Rugemarila awataja wezi wa fedha za Escrow
Leo January 5, 2017 Mfanyabiashara James Rugemarila anayekabiliwa na kesi ya utakatishaji fedha amewataja wezi wa fedha za Escrow katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kama alivyodai awali kuwa atawataja.
Wezi hao amewataja mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada ya Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU, Leornad Swai kueleza upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, hivyo anaomba iahirishwe hadi tarehe nyingine.
“Mwizi ni Standard Chartered Tanzania Ltd na Standard Chartered Hong Kong ambao wameisababishia serikali hasara ya Trilioni 37, pia nimewapelekea TAKUKURU washiriki wengine wa fedha hizo, hivyo ninaomba niendelee kuwa hai ili nije kuwa shahidi mzuri wa upande wa mashtaka kuhusu wezi hao.” – James Rugemarila
Pia Rugemarila amedai kuwa wezi hao ndio wamemuibia hata kwenye kampuni anayoisimamia ya VIP ambayo inawadai Trillion 16. Wakili Swai alidai kuwa ni kweli Rugemarila aliwasilisha taarifa ofisini kwao na wanazifanyia kazi kisha watatoa majibu.
Tofauti na hayo Rugemarila pia ameiomba mahakama imkubalie akafanyiwe uchunguzi nchini India kwa sababu anasumbuliwa na ugonjwa wa saratani kwa miaka 9 sasa huku mshtakiwa mwingine ambaye ni mmiliki wa IPTL Harbinder Singh Sethi aliiambia Mahakama kuwa tatizo lake la ugonjwa linajulikana.
Kutokana na hatua, Hakimu Simba amesema afya za washtakiwa ni muhimu hivyo wafanyiwe uchunguzi, pia anautaka upande wa mashtaka ukamilishe upelelezi kwa wakati, ambapo ameahirisha kesi hiyo hadi January 19,2018.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment