Thursday, January 4, 2018

Aliyeshinda unaibu meya aeleza alivyobebwa



Siku moja baada ya kufanikiwa kutetea nafasi ya unaibu meya wa jiji la Dar es Salaam, Mussa Kafana ameeleza namna alivyochukuliwa nyumbani kwake na kupelekwa kupiga kura akiwa mgonjwa.

Uchaguzi huo, uliokuwa na mchuano mkali kwa  kila upande kuwa na wajumbe 11 kwa 11 ulifanyika jana Jumatano katika ukumbi wa mikutano wa Karimjee na Kafana aliibuka kidedea kwa kupata 12 dhidi ya 10 alizopata Mariam Lulida wa CCM.

Akizungumza na gazeti hili leo Alhamisi, Januari 4, 2018, Kafana ambaye ni Diwani wa Kiwalani (CUF), amesema jana Jumatano alikuwa katika hali mbaya kiafya kwa kuwa alikuwa akisumbuliwa na malaria, kifua na tumbo la kuhara.

Amesema baada ya kuwa na hali hiyo, alitoa taarifa kwa ofisi ya mkurugenzi wa jiji la Dar es Salaam, ambayo iliamuru kutuma mwakilishi kwa ajili ya kuthibitisha kama anaumwa.

“Alikuja mwakilishi kutoka ofisi ya mkurugenzi ambaye alikwenda hadi katika zahanati niliyokuwa nikitibiwa na kupata uthibitisho, kisha akaja nyumbani kwa kupiniga picha  vyeti  na kuniona,” amesema Kafana.

Kafana amesema akiwa amepumzika baada ya kutoka hospitali  kadri muda ulivyokwenda simu zilikuwa zikipigwa kwa ndugu zake zikieleza kuwa anatakiwa kwenda kupiga kura hata kama ni mgonjwa na kwamba uchaguzi  hauwezi kuahirishwa.

“Waliwapigia ndugu zangu kwamba wanakuja kunichukua na wakahakikishia wasiwe na wasiwasi kila kitu kitakwenda sawa. Haukupita muda alikuja Kubenea (Saed –Mbunge wa Ubungo) na vijana wengine kunichukua mkukuku.

“Ule mwendo haukuwa wa kawaida, gari lilikimbia sasa kuhakikisha nashiriki uchaguzi. Ingekuwa jambo hili ni la mgombea binafsi nisingeenda kwa sababu nilikuwa najisikia vibaya, lakini wajumbe wenzangu wa Ukawa wakasema haiwezekani lazima nishiriki hata kama mgonjwa,” amesema Kafana.

Hata hivyo, jana Jumatano baada ya kuingia katika ukumbi wa mikutano Kafana hakuweza kupiga kura badala yake alisaidiwa na Kubenea ambaye alikuwa kiongozi kwa upande wa wajumbe wa Ukawa.

Kafana amesema alikuwa na uhakika wa kuibuka kidedea kutokana na idadi ya namba za wajumbe wanaounda Ukawa, lakini kutokana wajumbe wenzake kumhitaji ilimlazimu kuitikia wito huo huku akiwa taaban.

“Nilikuwa najiamini katika uchaguzi ule kutokana na uhusiano mzuri uliopo kati yangu na wajumbe wa Ukawa na CCM. Ndiyo maana sikushangaa kusikia kupigiwa kura na mmoja wajumbe kutoka CCM,” amesema Kafana.

Kuhusu madai ya yeye kuigiza mgonjwa wakati ni mzima wa afya, Kafana amesema “Mimi ndiyo mgonjwa nawashangaa hao wanaosema mimi ni mzima. Isingekuwa wajumbe wa Ukawa kunitaka niende,binafsi nisingeshiriki kwa kwenda na hali ile ni kujidhalilisha,” amesema.

Kafana ametumia nafasi kuwashukuru wajumbe wenzake kwa kumuwezesha kutetea nafasi hiyo na kwamba, alijua ungekuwa uchaguzi wa kawaida lakini kumbe ni kinyume.

Katika uchaguzi huo, mameya wawili Boniface Jacob (Ubungo-Chadema) na Abdallah Chaurembo (Temeke-CCM), nusura wazichape wakati wa shughuli ya kuhesabu kura, kama si wajumbe wa uchaguzi huo kuwatenganisha.

 Source: Mwananchi

No comments:

Post a Comment