Saturday, January 13, 2018
MICHIRIZI YA DAMU – 16
Akapelekwa katika chumba ambacho alitakiwa kukaa kwa siku zote ambazo angesubiri safari ya kwenda nchini Marekani. Moyo wa Fareed ulikuwa na furaha tele, hakuamini kama kweli alikutana na familia ya watu waliokuwa na upendo mkubwa kama watu hao.
“Jisikie huru!” alisema mzee huyo.
“Nashukuru sana!”
Mzee Al Fakh akaondoka na kwenda chumbani kwake, alipofika, haraka sana akachukua simu yake na kupiga namba fulani. Baada ya kupokelewa tu akaanza kuongea na mtu aliyekuwa upande wa pili.
“Nimefanikiwa kumpata mmoja, anaonekana kuwa na hamu ya kufika nchini Marekani! Ndiyo! Sasa huyo ndiye tutakayembebesha mabomu kwenda kulipua jijini New York katika kituo cha treni cha Pennsylvania. Haina shida, ataingia kama kawaida na hakuna ambaye atamshtukia, wasiliana na Hassan Bin Latif umpe maelekezo ya kumpokea mtu huyu na kumuelekeza ni kitu gani anatakiwa kufanya. Inshallah!” alisema Mzee Al Fakh na kukata simu.
****
Zaidi ya watu hamsini walifariki dunia katika mgahawa mmoja huko Amsterdam nchini Uholanzi baada ya bomu kulipua eneo hilo lililokuwa limekusanya watu wengi. Hiyo ilikuwa taarifa iliyoishtua dunia, ilikuwa ni idadi kubwa ya watu kuliko milipuko yote ambayo iliwahi kutokea katika nchi za Ulaya.
Watu walikuwa wakiendelea kujitoa mhanga, lilikuwa tukio baya la kujitoa mhanga ambalo lilitokea mwaka huo. Watu walilalamika, kundi la kigaidi la Al Qaeda lilijitokeza hadharani na kutangaza kwamba wao ndiyo walikuwa wamehusika katika mlipuko huo.
Marekani ikachukia, kila siku ilijitahidi kupambana na ugaidi, magaidi walikamatwa na kupelekwa katika gereza lililojaa mateso la Guantanamo lakini ugaidi haukupungua. Watu wengi, hasa vijana wa Kiarabu walikuwa wakikamatwa, walifundishwa kufanya matukio ya kigaidi huku akili zao zikijengwa kisaikolojia kwamba kuua katika ugaidi hakukuwa dhambi bali ni kuitetea dini.
Vijana wengi wa Kiarabu wakaingia katika mkumbo huo, waliahidiwa mambo mengi kwamba familia zao zisingepata shida tena na kama wangejitoa mhanga siku hiyohiyo wangekuwa peponi, pembeni ya mtume wakifarijiwa kwa kazi kubwa waliyoifanya duniani.
Hiyo ndiyo ilikuwa mbinu nyepesi ya kuwapata vijana wengi na wakafanikiwa hivyo kujitoa mhanga. Dunia ilionekana kubadilika, amani ikapotea, nchi nyingi za Ulaya zikawa na hofu na watu kutoka Mashariki ya Kati kwamba hawakuwa watu wa kuaminika na muda wowote ule wangeweza kufanya mauaji.
Kwa kipindi kirefu kundi hilo la kigaidi likatamani kulipua Marekani. Walikumbuka jinsi walivyotumia ndege mwaka 2001, hawakutaka kuridhika hivyo kutamani kulipua tena kwani waliamini kwamba wanaonewa, walitaka kuyaondoa majeshi ya Marekani na Uingereza nchi mwao, kitu pekee kuonyesha kwamba walichukizwa na uwepo wao huko kilikuwa ni kuwalipua tu.
Hawakujua ni kwa jinsi gani wangeweza kuingia nchini Marekani. Waliwatumia watu wengi kwenda huko lakini ilishindikana, hata kabla hawajaingia nchini Marekani, walikamatwa na hivyo kufungwa katika gereza la Guantanamo. Walijiuliza ni sababu zipi ziliwafanya kukamatwa kirahisi namna hiyo na jibu pekee walilolipata ni kwa sababu waliwatumia Waarabu wenzao.
Ili kuingiza bomu nchini Marekani ilitakiwa kumtumia Mzungu au mtu mweusi, hawakujua wangewapata vipi, kwa Wazungu ilikuwa vigumu sana lakini kwa watu weusi halikuonekana kuwa jambo gumu hata kidogo.
Wakakutana nchini Uturuki, nchi pekee barani Ulaya ambayo walikuwa wakikaa kwa usalama kwa kuwa watu wa nchi hiyo walikuwa Waarabu wenzao. Hapo ndipo walipopanga mipango, wakawafuata watu weusi waliotaka kuingia Marekani, waliwaambia kwamba walikuwa tayari kuwasaidia lakini walipowaambia kuhusu mabomu, waliogopa.
Walipoteza watu wengi, wakaweka vikao na kuona kwamba hawakutaka kuwaambia lengo la kuingia nchini Marekani bali walitakiwa kubaki kimya, wawape mizgo ya mabomu pasipo wao wenyewe kujua.
Kitendo cha Fareed kupatikana kiliwapa uhakika kwamba mwanaume huyo angefanikiwa kuingiza mabomu nchini humo, mawasiliano yakafanyika na hivyo taarifa kupelekwa kwamba tayari kijana mmoja alikuwa amepatikana, kijana aliyekuwa na hamu ya kuingia nchini Marekani.
“Hata mimi ninao wawili huku,” alisikika kijana aliyeitwa Mohammed Mustapha, mwanaume aliyekuwa akipanga safari za kwenda nchi mbalimbali kulipua.
“Safi sana. Basi nitaomba uje kumchukua na huyu,” alisema Mzee Al Fakh.
“Haina shida.”
Fareed hakuwa na hofu, moyo wake ulifurahi mno kwa kuona kwamba hiyo ndiyo ilikuwa nafasi yake ya kuelekea nchini Marekani. Hakuhisi kama watu hao walikuwa wabaya waliotaka kumbebesha mabomu mpaka nchini MArekani.
Mzee Al Fakh alipokuwa akizungumza naye, aliongea kiupole mno kiasi kwamba wakati mwingine Fareed alihisi kwamba mzee huyo alikuwa malaika aliyejivisha mwili wa binadamu.
Akalala na siku iliyofuatia, Mustapha akafika nyumbani hapo ambapo akatambulishwa kwa Fareed na hivyo kumchukua tayari kwa kuondoka naye kuelekea sehemu na kupanga safari hiyo.
Nyumbani kwa Mustapha akakutana na wanaume wengine wawili ambao hao nao walitakiwa kuondoka nao kuelekea nchini Marekani, vijana hao walikuwa weusi kama yeye, walikuwa wametoka nchini Senegal na wao walitamani kuingia nchini Marekani na kufanya mambo yao.
Siku hiyo wakasalimiana, wakazoeana na kulala pamoja. Usiku walizungumza mambo mengi, kila mmoja alimwambia mwenzake jinsi alivyosumbuka mpaka kufika nchini Uturuki. Kila mmoja alipitia msoto mkali mpaka kufika hapo. Kila walipoongea, waliwashukuru Waarabu hao, walionekana kuwa watu wazuri waliokuwa na lengo la kuwasaidia kufika nchini humo.
Walikaa pamoja kwa siku mbili tu kisha wakachukuliwa na kupelekwa sehemu iliyokuwa na makontena mengi. Wakaambia kwa sababu walitaka kuzamia nchini humo ilikuwa ni lazima waingie kupitia makontena hayo ambayo kwa ndani kulikuwa na kiyoyozi ambacho kingewafanya kuwa salama kipindi chote hicho.
Humo ndani, waliwekewa mabegi madogo ya mgongoni ambayo yalikuwa na vitu ndani, hawakujua kulikuwa na nini ila waliambiwa kwamba ile ilikuwa ni mizigo ambayo walitakiwa kuipeleka sehemu fulani ambapo huko wangekutana na mtu ambaye angewaambia ni nini cha kufanya.
Kwa New York ambapo walitakiwa kwenda, waliambiwa kabisa kwamba safari yao ingekwenda mpaka katika kituo cha treni cha Pennsylvania kilichokuwa jijini New York, watakapofika hapo, kuna mtu angewafuata na kuzungumza nao kisha kuondoka zake.
Hilo halikuwa tatizo, walichokuwa wakikihitaji ni kufika nchini Marekani tu. Hawakupoteza muda safari ikaanza kuondoka hapo Uturuki kwenda nchini Marekani. Kwa usafiri wa meli hiyo, wangetumia mwezi mmoja njiani mpaka kufika huko.
“Mwezi mmoja?” aliuliza Fareed.
“Ndiyo!” alijibu Mustapha.
“Ni kipindi kirefu mno, kweli hatuwezi kutumia hata wiki moja au chini ya hapo?” aliuliza Fareed.
“Ila ni mbali sana.”
“Ndiyo! Ila mwezi mzima nao ni mwingi mno,” alisema Fareed.
Hawakuwa na jinsi, hakukuwa na uwezekano wa kuwahi huko, ilikuwa ni lazima watumie mwezi mzima mpaka kufika nchini humo. Hawakuwa na hofu, walichojua ni kwamba walikuwa katika mikono salama na kusingekuwa na tatizo lolote lile.
Hawakutaka kujiuliza sana kuhusu mabegi madogo ambayo waliambiwa kwamba ni lazima waingie nayo nchini Marekani na kukutana na mtu ambaye aliwaambia kwamba wangekutana naye. Walimwamini Mustapha, kila mtu ambaye walikutanishwa naye, walimwamini kwa asilimia mia moja.
Safari ikaanza, ilikuwa ni ndefu na yenye kuchosha mno lakini hawakujali. Wiki ya kwanza ikakatika wakiwa majini, ya pili, ya tatu mpaka ya nne bado walikuwa njiani kuelekea nchini Marekani kwa kupitia katika Bahari ya Atlantiki.
Baada ya kupita siku ishirini na nane, wakaingia katika Visiwa vya Puerto Rico ambapo walipokelewa kinyemela na Waarabu wengine na kupelekwa katika nyumba moja kubwa na kutulia huko.
Bado waliendelea kuwaona Waarabu kuwa watu wema, hawakujua mpango mzito waliokuwa nao watu hao, hawakujua kama walikuwa wakienda kutolewa mhanga pasipo wao kujua.
Hapo Puerto Rico walikaa kwa siku mbili kisha kuondoka na kuelekea nchin Cuba ambapo hapo wakakutana na Waarabu wengine waliowaunganisha kwa baadhi ya wanajeshi na kuambiwa lengo la watu hao kufika hapo.
Kutokana na uadui mkubwa baina ya Marekani na Cuba, mipango ikaanza kusukwa upya, ilikuwa ni lazima Marekani ilipuliwe kwa mara nyingine tena na watu hao ndiyo waliowafanyia mpango Fareed na wenzake kuingia nchini Marekani kinyemela kabisa, njia walizokuwa wakitumia Wacuba hasa wauza unga na kutulia jijini New York.
“Kesho mtaelekea katika Kituo cha Pennslyvania, hapo kuna treni itakuja, kuna mtu atawaletea tiketi na nyie kuondoka, popote mtakapokwenda mtajua kivyenuvyenu, cha msingi tumekwishawaleta Marekani, sasa kutafuta maisha ni juu yenu,” alisema Mustapha huku akiwaangalia.
“Tunashukuru sana!” waliitikia huku wakiwa na furaha.
“Kesho ndiyo mtakwenda. Jiandaeni!”
“Sawa.”
****
Mustapha aliwapanga vijana wake ambao walitakiwa kuwapokea wakina Fareed ambao ndiyo wangekwenda katika kituo cha treni cha Pennslyvania kwa ajili ya kulipua kituo hicho.
Siku ambayo ndiyo ingekuwa siku ya tukio, vijana wa Mustapha ambao ndiyo wangeyaseti mabomu hayo tayari walifika katika kituo hicho kwa ajili ya kuwasubiri vijana waliokuwa na mabomu kwa ajili ya kuyalipua pasipo wao wenyewe kugundua kitu chochote kile.
Wakati hayo yote yakiendelea, Fareed alikuwa katika chumba kimoja na vijana wenzake, walikuwa wamejiandaa kwa ajili ya kwenda kulipua kituo hicho cha treni pasipo kujua kama ndani ya mabegi hayo kuliwa na mabomu.
Baada ya kupewa kiasi fulani kama kuwalaghai kwamba sasa wangekwenda huko na kuanza maisha yao, wakaelekea nje ambapo wakapanda gari na Mustapha na kwenda katika kituo hicho. Hakukuwa mbali sana, hawakutumia muda mrefu wakafika ambapo moja kwa moja wakaingia ndani.
Hakukuwa na mtu aliyejua kitu chochote kile, kila aliyekuwa akiwaangalia, alijua kwamba watu hao walikuwa abiria kama wengine. Walijichanganya na watu wengine na wao kusubiri treni ambayo ingefika mahali hapo muda si mrefu.
Bango kubwa lililokuwa mahali hapo lilikuwa likionyesha dakika zilizokuwa zimebaki kabla ya treni hiyo kufika katika kituo hicho. Watu walijikusanya, bango hilo lilionyesha kwamba ziliokuwa zimebaki dakika tano tu kabla ya treni hiyo kuchukua abiria kwenye kituo hicho na kuondoka.
Kila mmoja macho yake yalikuwa yakiangalia saa yake, kwa Fareed, alikosa amani, wenzake walikuwa wakifurahi kwamba hatimaye maisha yao yangeanza nchini Marekani lakini kwake, kila dakika zilipokuwa zikienda mbele ndivyo alivyokuwa na hofu zaidi.
“Humu ndani ya mabegi kuna nini? Kwa nini hawakuturuhusu tufungue ili tuangalie? Kama kuna kitu kizuri, hivi kweli wasingependa tujue?” alijiuliza Fareed huku akijaribu kujiuliza juu ya kile kilichokuwa ndani ya begi.
Muda huo Mustapha alikuwa pembeni yao, macho yake yalikuwa katika saa aliyokuwa ameivaa. Huku zikiwa zimebaki dakika tatu hata kabla ya treni kufika, Mwarabu mmoja akafika mahali hapo na kusimama pembeni ya Mustapha na kuanza kuzungumza naye.
Fareed alisikika lakini hakufahamu watu hao walikuwa wakizungumzia mambo gani. Mwanaume huyo aliyekuwa akizungumza na Fareed alikuwa na kifaa kama rimoti mkononi mwake, hakujua kazi ya hicho ila kwa jinsi kilivyoonekana, alijua kwamba hakikuwa kitu kizuri.
“Guys! I think this is our last time to meet each other! Have the good journey,” (jamani! Nafikiri huu ndiyo mara ya mwisho kuonana sisi nanyi! Muwe na safari njema) alisema Mustapha huku akiwaangalia wanaume hao.
“Thank you sir,” (ahsante bwana mkubwa)
Mustapha na yule mwanaume hawakutaka kusubiri mahali hapo, wakaondoka mahali hapo na kuelekea nje ya kituo hicho. Fareed na wenzake wakabaki kituoni hapo wakiwa na mabegi yale yaliyokuwa na mabomu.
Bado kichwa chake kilikuwa na mawazo tele, alikuwa na maswali mfululizo juu ya kile kilichokuwa ndani ya mabegi yale. Hakutaka kuridhika, akawaaga wenzake kwamba anakwenda chooni kujisaidia na angarudi muda si mrefu.
Akaondoka harakaharaka, alipofika chooni, kitu cha kwanza kilikuwa ni kuliweka chini lile begi, zipu zilifungwa kwa kufuli ndogo alichokifanya ni kulichana, ndani, akakutana na mfuko mweusi na alipoufungua, macho yake yakatua katika bomu moja kubwa lililokuwa likiwaka kitaa chekundu.
“Mungu wangu!” alisema kwa mshtuko, ghafla akasikia huko nje treni ikiwa inaingia, muda ambao bomu hilo lilitakiwa kulipuliwa.
****
Mustapha na mwenzake wakatoka nje, wakaelekea kwenye gari lao huku akiwa na furaha tele. Moyo wake aliona kwamba alifanikiwa katika kile walichokuwa wamekipanga kwamba mabomu yalifika salama nchini Marekani na muda huo yalikuwa kituoni.
Wakalifuata gari lao na kutulia humo. Mudda wote macho yao yalikuwa katika saa zao huku masikio yao yakisikiliza kwa makini kile kilichokuwa kikiendelea katika kituo kile. Kama treni ingekuwa inaingia kituoni hapo, kusingekuwa na ugumu wa kujua hilo, wangesikia mlio wake na hivyo kukaa kwa sekunde chache, litakaposimama tu waweze kulipua bomu hilo.
“Muda unakwenda tu! Subiri tusubiri,” alisema Mustapha.
Walisubiri kwa dakika tatu tu wakasikia treni likiwa linaingia, hawakutaka kuwa na presha kubwa, walisubiri mpaka waliposikia limesimama na abiria kuanza kuteremka. Mwanaume aliyekuwa na Mustapha akachukua kirimoti kile kwa lengo la kulipua mabomu yale.
“في سبيل الله,” (kwa ajili ya Mungu) alisema mwanaume yule kisha kubonyeza kitufe kile.
“Puuuuuuuu…..” ilisikika milio ya mabomu makubwa matatu yaliyopuka ndani ya kituo hicho.
****
Bilionea Belleck alikuwa na kila kitu, kila siku alikuwa akikusanya fedha nyingi kutokana na biashara mbalimbali alizokuwa akizifanya. Aliingiza kiasi kikubwa cha fedha na kila siku katika maisha yake aliendelea kuogelea kwenye dimbi kubwa la utajiri.
Alipendwa kutokana na sura nzuri aliyokuwa nayo, alipendwa kutokana na utajiri mkubwa aliokuwa nao. Kila siku kazi yake ilikuwa ni kubadilisha wanawake, alikuwa akienda kununua wanawake barabarani na kwenda kufanya nao mapenzi.
Aliyazoea maisha hayo, hakutaka kutulia nyumbani, alikuwa mtu wa safari, kusafiri kuelekea Ufaransa, Uholanzi, Italia, kila alipokuwa ilikuwa ni lazima kulala na wanawake kitu ambacho alipenda kufanya katika maisha yake.
Hakumfikiria mtu aliyeitwa Fareed, kwake, alijua kabisa mtu huyo hakuwepo katika uso wa dunia, alikumbuka jinsi alivyowatuma watu na kwenda kumtupa baharini, tena hakutupwa huku wakiwa watu hao, alitupwa huku akishuhudia kitu kilichompa uhakika kwamba mtu huyo alikuwa chakula cha samaki mpaka muda huo.
Baada ya kupata sana pesa, hatimaye yeye kama bilionea alitakiwa kukutana na mabiliona wenzake nchini Ufaransa kwa ajili ya kujadili biashara zao, huo ulikuwa mkutano mkubwa ambao kwa bilionea kama yeye ilikuwa ni lazima kushiriki na kuangalia ni kwa namna gani wangeweza kufanikiwa zaidi katika biashara zao na kuweka ubia na mabilionea wa Kiarabu kwa ajili ya kupanua soko lao.
Kikao kikafanyika nchini humo, kilikuwa kizito, kikubwa ambacho kilitangazwa na vyombo mbalimbali vya habari. Kikao hicho kilitakiwa kuchukua wiki moja kwani kulikuwa na mada nyingi, na kwenye kila mada ilikuwa ni kuwapendelea wao na si watu masikini ambao waliwafanya kuwa hapo.
Kwa sababu machangudoa walijua kwamba mabilionea walikuwa wateja wao wakubwa, wakawa wanakusanyika nje ya Hoteli ya King Napoleon II kwa ajili ya kuwanunua na kwenda kulala nao.
Kama ilivyokuwa kwa mabilionea wengi, kila siku ilikuwa ni lazima kwa Bilionea Belleck kuchukua changudoa na kuondoka naye kulala naye usiku mzima. Alikuwa na pesa, alikuwa na kila kitu alichokuwa akikihitaji katika maisha yake, hakuona kama kulikuwa na ugumu wa kulala na mwanamke yeyote aliyekuwa akimuhitaji katika kipindi hicho.
“Unaitwa nani?” aliuliza mara baada ya kumfuata msichana mmoja kisri.
“Natalie!”
“Ooh! Gharama zako zipo vipi?”
“Euro elfu moja!”
“Sawa!”
Hakuwa na mazungumzo marefu, alijiamini, hakuona kama kulikuwa na changudoa ambaye angemtajia gharama ya pesa ambazo hakuwa nazo. Akamchukua msichana huyo na kuondoka zake.
Hakutaka kuwa na wapambe, alitaka kufanya kila kitu peke yake, aliamini kwamba kama angekuwa na wapambe mambo yangevuja na hatimaye kujulikana kama alikuwa akinunua machangudoa kitu ambacho hakutaka kabisa kijulikane kwa kuogopa kumuumiza mkewe.
Machangudoa wengi walipenda kununuliwa na mzee huyo kwa sababu alikuwa na uhuru wa kukwambia wewe mwenyewe upange bei. Walipokuwa wakiliona gari lake, walilikimbilia na kujipanga mstari na hivyo kuchagua ni yupi alitakiwa kulala naye usiku wa siku hiyo.
Baada ya wiki moja kumalizika na mkutano huo kuisha, hakutaka kuondoka nchini Ufaransa, alitaka kuendelea kubaki mahali hapo kwani kulimteka, wanawake wazuri waliokuwa katika Jiji la Paris walimdatisha kichwa chake na hivyo kutamani kuendelea kukaa zaidi.
****
Kila kitu alichokuwa akikifanya ndani ya choo kile, Fareed alikifanya harakaharaka, hakutaka kuchelewa kwani kwa jinsi bomu lile lilivyoonekana, halikuwa limebakiza dakika nyingi kulipuka.
Akaliacha begi palepale chini na kisha kukimbia kutoka chooni hapo, hakutaka kubaki ndani ya kituo hicho kwani aliamini kwamba endapo angebaki basi naye pia angeweza kufa.
Kila mtu alibaki akimshangaa, wengine walihisi kwamba alikuwa mwizi, kwamba aliiba na hivyo kukimbia. Sehemu ambayo ilikuwa ikijifungua kwa kichuma kwenda juu baada ya kuweka tiketi, hakutaka hata ijifungue, akaruka kwa juu na kuelekea nje.
Wakati anafika nje ya kituo hicho kwa kupitia mlango mwingine, mabomu yakasikika yakilipuka na nguvu yake ilikuwa kubwa kiasi kwamba mpaka wao waliokuwa nje ya kituo kile wakarushwa akiwepo yeye mwenyewe.
Akaangukia katika gari moja lililokuwa limepaki pembeni, watu wengine waliokuwa hapo walikuwa hoi, wengine walikuwa wakiteketa kwa moto, pale alipoangukia ambapo kulikuwa ni kama hatua kumi kutoka pale alipokuwa amefikia, Fareed alikuwa hoi, kichwa chake kilikuwa kikitoka damu, alisikia maumivu makubwa mwilini mwake.
Akajitahidi kusimama, akashindwa, akabaki hapohapo akiwa amelala huku macho yake yakiwa mazito kabisa. Akajitahidi kuuinua mkono wake, akashindwa, kila kitu alichotaka kukifanya mahali hapo alishindwa kabisa.
Kwa kutumia uangaliaji wake wa kwa mbali, akawaona watu wakikimbia huku wakipiga kelele za kuomba msaada, baada ya sekunde ishirini tu akiwa hapo, giza kubwa likayafumba macho yake na baada ya sekunde hizo, akapoteza fahamu na hakujua kitu gani kiliendelea.
****
Lilikuwa tukio kubwa lililoishtua dunia, hakukuwa na mtu aliyeamini kama kweli Marekani ingeweza kulipuliwa kama ilivyotokea. Kila mtu alishangaa kwani kwa jinsi nchi hiyo ilivyokuwa imejiwekea ulinzi tangu kulipuliwa kwa maghorofa ya biashara ya WTC, hakukuwa na aliyeamini kwamba kweli magaidi wangeweza kuilipua nchi hiyo kwa mara nyingine.
Watu zaidi ya elfu moja mia tano wakasadikiwa kufa katika tuki hilo huku maelfu wakijeruhiwa vibaya. Ndani ya dakika chache tangu tukio hilo litokee, magari ya zimamoto yakafika mahali hapo yakiongozana na magari kadhaa ya wagonjwa.
Polisi wakaweka kamba ya nyano iliyoandikwa ‘Do not cross’ yaani Usivuke huku ni polisi tu na watu wa afya ndiyo walioruhusiwa kwenda ndani ya kituo kile kulipotapakaa miili mingi ya watu.
Mambo yote hayo yalikuwa yakiendelea huku Fareed akiwa chini, hakujitambua, pale alipokuwa, kwa jinsi alivyokuwa amerushwa, ilikuwa vigumu kuamini kama mtu huyo alikuwa mzima.
Yeye na majeruhi wengine wakachukuliwa na kukimbizwa hospitali kwa ajili ya matibabu huku nyuma waandishi wa habri wakiendelea kukusanyika katika eneo hilo la tukio kwa ajili ya kuripoti kila kitu kilichokuwa kikiendelea.
Gari halikuchukua muda mrefu likafika katika Hospitali ya St. Joseph Medical Centre iliyokuwa hapohapo Pennsylvania ambapo mara baada ya magari kuingizwa ndani, machela zikaletwa, majeruhi wakapandishwa kwenye machela hizo kisha kupelekwa ndani.
Hiyo ndiyo ilikuwa siku ya kwanza kwa Fareed kukaa ndani ya hospitali hiyo. Matibabu yalikuwa yakiendelea kama kawaida. Baada ya saa kumi na mbili, akarudiwa na fahamu, akayafumbua macho yake na kuanza kuangalia huku na kule.
Mahali pale palikuwa ni hospitali, hakujua alikuwa amefikaje, aliangalia huku na kule, kwa juu, dripu ilikuwa ikining’inia huku mwili wake ukiwa na maumivu makali kiasi kwamba alishindwa hata kugeuka.
Mbali na yeye, ndani ya wodi ile kulikuwa na wagonjwa wengine ambao hawakuonekana kuwa na nafuu kama alivyokuwa. Huo haukuwa mwisho wa safari yake, ilikuwa ni lazima aondoke mahali hapo, alitaka kwenda sehemu kwa ajili ya kukaa kisha kumtafuta Bilionea Belleck ambaye aliamini kwamba bado alikuwa hapohapo Marekani.
“Ni lazima niondoke hapa,” alisema Fareed.
Kuondoka mahali hapo haikuwa kazi nyepesi, mara kwa mara madaktari na manesi walikuwa wakifika kwa ajili ya kuangalia maendeleo yao. Hakutaka kabisa kuendelea kubaki kwani bado maisha yake aliyaona kuwa na hatari kubwa.
Kwa kuwa kulikuwa na ugumu wa kufanya hivyo, kitu chepesi alichokifanya ni kusubiri mpaka usiku ambapo akaomba nafasi ya kwenda chooni kwa lengo la kufika huko na kukimbia zake.
Akasimama na kutembea kwa mwendo wa taratibu, mwendo ulioonyesha kwamba hakuwa mzima kiafya, alipofika chooni, akajisaidia haja ndogo na kuangalia ni kwa namna gani angeweza kutoroka hospitali hapo pasipo kuonekana.
**
Bado watu waliendelea kushangaa juu ya tukio la kigaidi lililokuwa limetokea nchini Marekani. Shirika la kipelelezi la FBI lilikuwa kwenye wakati mgumu, hawakujua ni kwa jinsi gani wangeweza kuwapata wahusika wakuu wa tukio hilo ingawa Al Qaida walijitokeza hadharani na kusema kwamba wao walihusika kwa kila kitu.
Walichokuwa wakikihitaji FBI ni picha zilizokuwa zimepigwa dakika kadhaa kabla ya tukio kutokea. Ilikuwa ni lazima waangalie kwenye kamera za CCTV kuona kila kitu kilichokuwa kimetokea humo.
Wakaelekea katika chumba kilichokuwa na kompyuta nyingi, zilikuwa zimeunguzwa vibaya lakini walichoshukuru Mungu ni kwamba memory cards zote ambazo zilikuwa zimechukua picha kutoka ndani ya kituo hicho kabla ya tukio la kmlipuko kutokea, zilikuwa salama kabisa.
Wakazichukua na kuelekea katika kompyuta zao na kuangalia kuona kama wangeweza kuwaona wahusika wa mlipuko ule. Walifanikiwa kumuona Fareed na wenzake, waliwahisi kwamba hawakuwa na nia nzuri kutokana na mabegi ya kufanana waliyokuwa nayo. Baada ya dakika kadhaa, wakamuona Fareed akiondoka.
“Let’s roll with him,” (twende naye huyo) alisema Frankline, mmoja wa FBI waliokuwa wakifuatilia tukio hilo.
Kwa kutumia kamera mbalimbali waliweza kumfuatilia Fareed aliyekuwa akikimbia, alipofika chooni, akaingia na kisha kutoka na kuendelea kukimbia. Wakahisi kwamba huyo ndiye aliyekuwa amehusika na mlipuko ule, wakaendelea kumfuatilia mpaka nje, kituo kikalipuka, na yeye mwenyewe akarushwa na kujipigiza katika gari moja.
“Take his picture,” (chukua picha yake) alisema Frankline na mwenzake kufanya hivyo, walivyoikuza, wakamgundua, picha ikaprintiwa na mpaka gari la wagonjwa lilipomchukua na kuondoka naye, walikuwa wakifuatilia kila kitu.
“Which hospital?” (hospitali gani?)
“St. Joseph!”
“Let’s go…let’s go,” (twendeni…twendeni) alisema Franckiline, maofisa wanne wa FBI waliokuwa na bunduki wakaanza kwenda kwenye hospitali hiyo kwa ajili ya kumkamata Fareed ambaye walikuwa na uhakika kwamba alihusika kwa asilimia mia moja katika mlipuko huo.
Wakawapa wenzao taarifa juu ya kile kilichokuwa kimetokea, hawakuishia kuwataarifu bali wakawatumia na picha za mwanaume huyo na kwamba walikuwa njiani kwenda kumkamata.
Kwa kuwa mahali hapo hakukuwa mbali na hospitali, ndani ya dakika kumi wakafika na moja kwa moja kuingia ndani. Kulikuwa na idadi kubwa ya watu, wengi waliokuwa mahali hapo walifika kwa ajili ya kuwaona ndegu zao waliokuwa hoi.
Wakazungumza na madaktari na kumuonyeshea picha ya Fareed, kwa kuwa daktari huyo alikuwa akiwakumbuka watu aliokuwa amewapokea, hakukuwa na ugumu kugundua kwamba picha ya mtu aliyekuwa ameonyeshewa alikufikishwa ndani ya hospitali hiyo saa moja iliyopita.
“Where is him?” (yupo wapi?)
“Come with me,” (nifuateni) alisema daktari huyo na kuanza kumfuata.
Daktari yule akawapeleka mpaka katika wodi aliyolazwa Fareed ambapo akawakabidhi watu hao kwa nesi aliyekuwa akiwahudumia wagonjwa waliokuwa katika wodi hiyo. Alipoonyeshewa picha ya Fareed, alimgundua kwani alikuwa miongoni mwa wagonjwa waliokuwepo humo ndani.
“I know him,” (namfahamu)
“Where is he? (yupo wapi?)
Nesi yule akawachukua mpaka katika kitanda alicholazwa Fareed, walipofika, mwanaume huyo hakuwepo na alipomuuliza nesi mwenzake akamwambia kwamba Fareed alikuwa amekwenda chooni.
“Where is the toilet?” (choo kipo wapi?)
“Come with me,” (nifuateni) alisema na kuanza kumfuata nesi huyo kwenda huko chooni.
****
Maofisa wale wa FBI na nesi yule wakafika ndani ya choo kile, wakaangalia huku na kule, mtu waliyekuwa wakimtafuta hakuwepo humo. Nesi alishindwa kuelewa kwamba ilikuwaje Fareed asiwe humo na wakati alimuona akielekea chooni na hakuwa na uhakika kama mwanaume huyo alikuwa ametoka.
FBI hawakutaka kuridhika, walijua kwamba mwanaume huyo alikuwa ndani ya vyoo hivyo, wakaendelea kumtafuta kwenye kila choo lakini hawakuweza kumuona.
Hawakutaka kukata tamaa, waliamini kwamba kama mwanaume huyo hakuwa chooni humo basi atakuwa ametoka, na kama ni kipindi kifupi kilichopita waliamini kwamba hakuwa mbali kutoka mahali hapo.
Wakaelekea sehemu zingine ndani ya hospitali hiyo lakini hawakuweza kumuona Fareed, wakaelekea mpaka nje kabisa lakini kila kona waliyoangalia, mwanaume huyo hakuonekana machoni mwao.
“Where is he?” (yupo wapi?) aliuliza ofisa mmoja.
“I don’t know! He just went to the toilet,” (sijui! Alikwenda chooni) alijibu nesi.
****
Fareed alikuwa chooni, moyo wake haukuwa na amani hata kidogo, aliamini kwamba ilikuwa ni lazima kutafutwa kwani alikumbuka kwamba katika kituo kile cha treni kulikuwa na kamera ndogo za CCTV hivyo kugundulika lilikuwa suala jepesi sana.
Hakutaka kubaki humo, ilikuwa ni lazima kuondoka kuelekea popote pale lakini si kuona akikamatwa kwa kufanya jambo ambalo alilazimishwa kulifanya pasipo kujua kama lilikuwa kosa lolote lile.
Akaondoka na kuelekea nje ya choo kile, hakutaka kuonekana, aliondoka mpaka kufika nje huku akikutana na madaktari wengi ambao hawakumuuliza kitu chochote zaidi ya kumuacha tu.
Alijipekua mfukoni, alikuwa na kadi yake ya benki ambayo ilimuwezesha kuchukua kiasi chochote cha pesa sehemu yoyote ile. Akaelekea mpaka katikakibanda cha ATM na kutoa kiasi cha dola mia tano na kuondoka zake.
Safari yake iliishia katika hoteli ya kawaida ya Windows iliyokuwa hapohapo Pennyslvania, akachukua chumba ambacho alitakiwa kulipa dola mia mbili hamsini, zaidi ya laki tano kwa usiku mmoja tu.
Hilo halikuwa na tatizo, alikuwa na kiasi kikubwa cha fedha ambacho angeweza kufanya jambo lolote lile, hivyo akaelekea katika chumba hicho. Hakulala, alibaki akifikiria namna alivyonusurika kuuawa kwa kulipukiwa na bomu.
Moyo wake ukawa na ghadhabu, akawa na hasira na Waarabu kwani aliamini kwamba watu hao hawakuangalia utu, hawakujua ni watu wangapi waliwakosea, katika kuua, waliua kila mtu hata kama hawakuwa na hatia kama alivyokuwa.
Hakutaka kuwafikiria sana Waarabu, alichokitaka ni kusonga mbele na kutekeleza kile alichokuwa akikitaka. Aliingia nchini MArekani kwa lengo la kumuua Bilionea Belleck ambaye aliamini kwamba alikuwa nchini humo.
Akaanza kufuatilia, alikuwa na marafiki wachache nchini humo ambao wangekuwa na data zote kuhusu bilionea huyo na kwa jinsi gani angeweza kumpata. Kwa kuwa bilionea Belleck alikuwa na maadui wengi akiwemo bilionea mwenzake, Peter Williams, alichokifanya ni kumpigia simu.
“Unanikumbuka?” alimuuliza bilionea huyo ambaye aliwahi kutambulishwa na Bilionea Belleck kabla ya wawili hao kutofautiana kwenye mambo ya kibiashara.
“Hapana!”
“Kwa hiyo namba yangu uliifuta?” aliuliza Fareed.
“Mmh! Sina uhakika! Wewe nani?”
“Naitwa Farida!”
“Yupi?”
“Yule wa Belleck!”
“Ooh! Yule wa mpumbavu?”
“Ndiyo!”
Kwa sababu watu hao walikuwa wakichukiana, Fareed aliamini kwamba angeweza kufanya naye kazi kwa ajili ya kukamilisha kile alichokuwa akikihitaji. Akamwambia mwanaume huyo kwamba walitakiwa kuonana na hivyo kama hatojali basi aende kuzungumza naye kitu ambacho kwa bilionea huyo hakukuwa na tatizo lolote lile.
Ndani ya saa moja tayari Bilionea William alikuwa mbele ya Fareed. Alimwangalia kwa umakini sana, alionekana kuwa mtu tofauti kabisa, hakuwa kama kipindi kilichopita, mwanaume mwenye muonekano wa kike, kwa kipindi hicho alikuwa mwanaume shupavu, mwenye mwili uliojazia.
Williams alibaki akimkodolea macho, hakuamini kama mwanaume aliyesimama mbele yake ndiye mwanaume yule aliyefahamiana naye kitambo. Fareed akamwambia bilionea huyo kile kilichomleta Marekani, hakuja kula starehe bali alitaka kufanya kazi moja, kumuua Bilionea Belleck.
“Kwa nini tena?”
Akamwambia sababu kwamba aliamua kufanya hivyo kwa kuwa mwanaume huyo naye alitaka kumuua ila kwa msaada wa Mungu aliweza kumtoroka na watu wake.
Williams akafurahia, chuki aliyokuwa nayo kwa Belleck ilikuwa kubwa kiasi kwamba kwa kitendo cha kuambiwa kwamba mwanaume huyo alikuwa tayari kumuua halikuwa tatizo kabisa.
“Kwanza hayupo Marekani,” alisema William.
“Yupo wapi?”
“Paris nchini Ufaransa,” alijibu Williams.
“Ni lazima niende huko. Utanisaidiaje kufika?” aliuliza Fareed.
Ili apate msaada wa kufika Ufaransa ilikuwa ni lazima amwambie Williams ukweli kwamba alikuwa akitafutwa kila kona. Mwanaume huyo alibaki kimya, alitaka muda wa kujifikiria ni kwa jinsi gani angemtorosha Fareed kuelekea nchini Ufaransa.
Alikaa na kuwaza sana, jibu alilokuja nalo ilikuwa ni lazima kwa mwanaume huyo asafiri kwa kutumia ndege yake binafsi ambayo ingempeleka mpaka huko.
“You will take my flight,” (utachukua ndege yangu) alisema Williams.
Hakuwa na uamuzi mwingine zaidi ya huo na safari ilitakiwa kufanyika usiku. Fareed akajiandaa na baada ya siku mbili, magari mawili ya kifahari yakafika hotelini hapo na kumchukua kisha kumpeleka uwanja wa ndege.
Moyo wake ulikuwa na hofu, hakuamini kama angefika salama huko kwani kila kona alikuwa akitafutwa na FBI ambao hawakutaka kuzisambaza picha zake, walimtafuta kimyakimya ili asishtukie kama anatafutwa kumbe mwenzao alikwishajua hilo kitambo.
Uwanja wa ndege, hakupitishwa mlango wa kawaida, ndege ilikuwa ni ya binafsi tena ya bilionea mkubwa duniani, hivyo hata mlango aliopitishwa ulikuwa ni wa VIP na ilikuwa vigumu kumgundua kwamba alikuwa yeye.
Mpaka anakaa katika kiti ndani ya ndege hiyo, akashusha pumzi ndefu, hakutegemea kama ingekuwa kazi nyepesi namna hiyo. Huku nyuma, bilionea Williams alikuwa akifanya mawasiliano na watu wake waliokuwa Ufaransa, alitaka kupata data zote kuhusu bilionea huyo, kwamba alikuwa akiishi katika hoteli gani na ratiba yake ya siku ilikuwaje. Hilo halikuwa tatizo kwa vijana wake, kwa kuwa walikuwa huko na mtu huyo alikuwa maarufu, wakapata data zote na kumtumia na hivyo na yeye kumtumia Fareed ambaye baada ya kuzipokea, akamshukuru Mungu.
“Sasa kazi itafanyika,” alimwambia Williams kwenye simu.
“Ukikamilisha! Nakuahidi kukupa dola milioni kumi. Huyu mpumbavu ananinyima sana usingizi,” alisema William huku akiwa na uhakika kwamba ilikuwa ni lazima mwanaume huyo ammalize Bilionea Belleck. Ila la zaidi, alitaka kuona bilionea huyo akifa na yeye kumuua Fareed kwani kama angemuacha, siri ingeweza kuvuja. Ili siri itunzwe ilikuwa ni lazima hata naye Fareed afe.
****
Fareed hakujua mahali mwanaume huyo alipokuwa, ila aliambiwa kwamba angepewa maelezo yote kwani yale aliyopewa mara ya kwanza, yalibadilika kwani mtu huyo aliondoka Paris na hakukuwa na aliyejua kama alikwenda Monaco au Marseille.
Baada ya dakika hamsini akapigiwa simu na kuambiwa kwamba mwanaume huyo hakuwa hapo Paris bali alikuwa jijini Marseille katika Hoteli ya Melkizedeki ambapo alikuwa akilala huku kila siku akishiriki katika kikao cha matajiri.
Hilo halikuwa tatizo, haraka sana akaondoka hotelini alipokuwa, akachukua ndege na kuelekea Marseille ambapo ndipo aliambiwa mwanaume huyo alipokuwa. Njiani, alikuwa akimuomba Mungu afike salama kwani alikuwa na hasira kali, asingeweza kumuacha mwanaume huyo akaishi kwani alikuwa miongoni mwa watu waliotaka kumuua kwa nguvu zote.
Walichukua dakika arobaini na tano tu mpaka kufika jiji humo ambapo akateremka na kuchukuliwa kwa gari mpaka katika hoteli moja na kutulia huko. Ilipofika saa mbili usiku, wanaume wawili wakafika hotelini hapo na kuomba kuzungumza naye.
Hilo halikuwa tatizo, alipewa taarifa na Williams kwamba watu hao wangefika mahali hapo, na wao ndiyo ambao wangemwambia kuhusu Belleck ambaye hakujua alikuwa katika hoteli gani.
“Belleck yupo anakula raha, hivi tunavyoongea, keshokutwa anaondoka kurudi Marekani,” alisema mwanaume mmoja aliyejitambulisha kwa jina la De Leux.
“Sawa. Kingine?”
“Huwa anapenda sana kununua malaya mitaani! Tunajua sehemu ambayo hupenda kununua na pia tunajua hoteli anayokaa mpaka chumba alichokuwepo,” alisema De Leux.
“Haina shida! Ningependa nikutane naye na kufanya kazi yangu,” alisema Fareed.
Hakwenda huko kufanya jambo lolote zaidi ya kumuua bilionea huyo na kuondoka zake. Wanaume hao wawili ndiyo walikuwa wachora ramani wakubwa, walikuwa wakienda hotelini hapo, wanaonana na wahudumu wa hapo, wakatengeneza urafiki wa kizushi kwa ajili ya kuwasaidia hapo baadaye.
Hawakujua kama lengo la watu hao ni kumpata mwanaume aliyekuwa ndani ya hoteli hiyo. Wakati mwingine walikuwa wakikaa mapokezini, Belleck alipokuwa akiingia ndani ya hoteli ile na machangudoa walikuwa wakimuona hivyo kuwa kazi nyepesi kwao kufanya kile walichokuwa wakikitaka.
“Cha kwanza ni kupata kadi ya kufungua vyumba vyote,” alisema De Leux.
Hilo ndilo lililotakiwa, kwa kutumia uzoefu mkubwa wa kuzungumza waliokuwa nao, wakajenga ukaribu zaidi na mhudumu aliyeitwa kwa jina la Natalie ambaye bila tatizo lolote lile, naye akaukaribisha ukaribu huo na mwisho wa siku De Leux kumtongoza.
“Acha masihara wewe! Mzuri mimi?” aliuliza Natalie huku akitabasamu, japokuwa alipinga kwamba hakuwa mzuri lakini sifa zile zilimfurahisha.
“Wewe ni mzuri sana. Una tabasamu pana, msichana mrembo sana! Umeumbinka kama Mona Liza,” alisema De Leux huku akimwangalia Natalie kwa macho ya nipe nikupe.
Akamsifia usiku mzima, msichana huyo akachanganyikiwa, kila wakati akawa anapandisha juu mpaka katika chumba alichokuwa akilala De Leux na kuingia ndani. Hakutaka kufanya mapenzi na msichana huyo, kitu muhimu kilikuwa ni kuweka ukaribu na mwisho wa siku kuichukua kadi ambayo alikuwa akiitaka mno.
Wakati walipokwenda kuonana na Fareed, walimwambia kabisa kile kilichokuwa kimetokea kwamba kulikuwa na kadi moja muhimu ambayo ingewawezesha wao kuingia ndani ya chumba chochote kile.
Fareed akafurahi kwani urahisi huo ndiyo aliokuwa akiutaka kwa hali na mali. Siku hiyo wakaondoka na kwenda katika hoteli hiyo. Wakachukua chumba kwa ajili ya Fareed ambaye akaingia bila tatizo na uzembe mkubwa ambao waliufanya wahudumu wa hoteli hiyo ni kutokuishikilia passport yake.
Akaingia mpaka chumbani, akajipumzisha na kuambiwa kwamba mtu aliyetakiwa kumuua alikuwa njiani kufika mahali hapo hivyo alitakiwa kusubiri.
De Leux na mwenzake wakarudi mapokezi, wakatulia kochini. Ilipofika saa sita usiku, wakamuona Belleck akirudi hotelini hapo huku akiwa na mwanamke ambaye alivalia hijabu ila kwa nyuma alijazia hasa kiasi kwamba hata wao walipokuwa wakimwangalia walimtamani kupita kawaida.
“Huyo hapo! Subiri!” alisema De Leux.
Wakati mwanaume huyo akiingia ndani na mwanamke huyo, De Leux akamuita Natalie na kuanza kuongea naye. Alimwambia wazi kwamba siku hiyo alitaka kukaa naye na kuzungumza naye mambo mengi lakini iwe baada ya kufanya usafi katika vyumba mbalimbali.
“Haina shida mpenzi! Nitakuja,” alisema Natalie huku akionekana kuwa na furaha tele.
De Leux akaondoka na mwenzake mpaka chumbani kwake, wakakaa huko na kuyapanga kwamba siku hiyo ndiyo ilikuwa mwisho wa mtu huyo ambaye alikuwa adui wa bosi wao kwa kipindi kirefu.
Wakamfuata Fareed na kumwambia kilichokuwa kikiendelea kwamba ni yeye tu ndiye aliyekuwa akisubiriwa kufanya mauaji hayo.
“Haina tatizo!”
“Sawa. Ngoja nimuite huyu msichana alete kadi,” alisema De Leux na hapohapo kuchukua simu ya mezani na kupiga mapokezi ambapo alimtaka Natalie aende huko kuchukua shuka kwenda kulifua.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment