Wednesday, January 3, 2018

Bodi ya Mikopo yatangaza vita kwa Wanafunzi waliokiuka sheria



Dar es Salaam. Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza kiama kwa wanufaika119,497 nchini kote ambao wamekiuka sheria iliyoanzisha bodi hiyo kwa kutoanza kurejesha mikopo yenye thamani ya Sh 285 bilioni waliokopeshwa tangu mwaka 1994/1995 na mikopo yao imeiva lakini hawajaanza kurejesha.

Taarifa iliyotolewa leo Jumatano imeeleza kuwa itaanza kuwasaka wanufaika hao kuwanzia Jumatatu, Januari 8, 2018.

Imeeleza kuwa inatarajia kuanza kufanya ukaguzi kwa waajiri mbalimbali nchini kote ili kubaini kama katika orodha za waajiriwa wao (payrolls) kuna wanufaika wa mikopo ambao hawajaanza kurejesha.

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru amesema Jumatano kuwa msako huo utafanywa kwa miezi mitatu kuanzia wiki ijayo Jumatatu, Januari 8, 2018.

Badru ametoa kauli hiyo wakati akitoa tathmini ya utekelezaji wa majukumu ya Bodi ya Mikopo kwa nusu ya mwaka wa fedha wa 2017/2018 uliomalizika Desemba 31, 2017.

Akifafanua zaidi, Badru amesemaingawa kila mwajiri ana wajibu wa kisheria wa kuwasilisha makato ya wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu kwa bodi ndani ya siku 15 baada ya mwisho wa mwezi, baadhi ya waajiri wamekuwa hawafanyi hivyo na kuilazimisha bodi hiyo kuanza kuwasaka kwa nguvu.

“Katika msako huu hatutamuacha mtu au mwajiri yeyote anayekiuka sheria iliyoanzisha bodi,” amesema Badru katika mkutano na wanahabari na kufafanua kuwa sheria iliyoanzisha Bodi ya Mikopo inawapa mamlaka ya kufanya ukaguzi na ni kosa kisheria kwa mtu yeyote kuzuia ukaguzi huo.

“Tayari tumeziongezea nguvu ofisi zetu za Kanda zilizopo Mwanza, Arusha, Dodoma na Zanzibar ili kuendesha ukaguzi na msako katika mikoa yao na ile iliyo karibu nayo ili kuhakikisha kazi hii inafanyika kwa ufanisi,” amesema Badru na kuongeza kuwa ukaguzi huo pia utafanyika jijini Dar es Salaam.


No comments:

Post a Comment