Friday, January 5, 2018

Korea Kaskazini yakubali mazungumzo kuhusu Olimpiki


Korea Kaskazini imekubali kushiriki mazungumzo ya ngazi ya juu wiki ijayo kuhusu kushiriki kwa wachezaji wake katika michezo ya Olimpiki ya majira ya baridi, Korea Kusini imesema.

Mkutano huo wa Januari 9 utaangazia kutafuta njia ya wachezaji wa Korea Kaskazini kushiriki michezo hiyo itakayoandaliwa Korea Kusini Februari.

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un alisema wiki hii kwamba atawatuma wawakilishi katika michezo hiyo na kusema hiyo itakuwa "fursa nzuri ya kuonyesha umoja" miongoni mwa raia wa Korea Kaskazini.

Mkutano huo unatarajiwa kufanyika Panmunjom, mpakani, Eneo hilo linalofahamika kama kijiji cha amani linapatikana katika eneo lisiloruhusiwa kuwa na wanajeshi mpakani, na ni hapo ambapo mazungumzo kati ya nchi hizo yamekuwa yakifanyika tangu zamani.

Kwa mujibu wa afisa kutoka afisi ya rais wa Korea Kusini, mkutano huo utaangazia zaidi michezo hiyo itakayofanyika Pyeongchang.

Hata hivyo, aliambia shirika la habari la Yonhap la Korea Kusini kwamba anaamini kutakuwepo pia na "mazungumzo kuhusiana na kuboresha uhusiano kati ya Korea Kusini na Korea Kaskazini baada ya kuthibitishwa kwa ushiriki wa Kaskazini katika michezo hiyo."

Hayo yatakuwa mazungumzo ya kwanza ya ngazi ya juu kufanyika kati ya nchi hizo mbili tangu Desemba 2015.

Haijabainika ni nani watashiriki mazungumzo hayo, Rais wa Korea Kusini Moon Jae-in alikuwa awali amesema anatazama michezo hiyo kama fursa mwafaka ya kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo mbili.

Mapema wiki hii, Korea Kaskazini ilirejesha mawasiliano ya simu maalum kati ya nchi hizo mbili, kufanikisha mazungumzo hayo.

Hata hivyo, afisa wa wizara ya Korea Kusini kuhusu kuunganishwa kwa mataifa hayo mawili alisema Korea Kaskazini ilikubali mwaliko wa kushiriki mazungumzo hayo kupitia kipepesi.


No comments:

Post a Comment