BEKI wa kati wa Yanga, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ amefunguka kuwa amewafunga midomo wale wote waliokuwa wanabeza uwezo wake huku wengine wakidhani angeweza kusababisha penalti katika mchezo wao dhidi ya Mbao, wikiendi iliyopita.
Ninja ambaye aliumia katika mchezo wa juzi wa Kombe la Mapinduzi dhidi ya Mlandege, alijiunga na Yanga kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Taifa Jang’ombe ya Zanzibar.
Wikiendi iliyopita, Ninja alicheza mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu Bara tangu ajiunge na timu hiyo ambapo timu yake ilipoteza kwa kufungwa mabao 2-0 dhidi ya Mbao.
Ninja amefikia hatua ya kusema hivyo baada ya kwenye mechi za kirafiki alizocheza huko nyuma akiwa na jezi ya Yanga, kusababisha penalti huku akijifunga wakati timu hiyo ikijiandaa na msimu huu ambapo mashabiki wa timu hiyo walikuwa wakimsema mitandaoni kwa kucheza hovyo.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Ninja alisema kuwa, wikiendi iliyopita muda mfupi baada kikosi kutoka na jina lake kuwepo, alipatwa na hofu kubwa kutokana na mashabiki kuanza kusema vibaya mitandaoni wakiamini atasababisha penalti lakini anashukuru ikawa tofauti na matarajio yao.
“Kwanza nashukuru nimeanza kucheza lakini nilipata na hofu ambayo ikanipa ujasiri mkubwa kwa sababu mashabiki walianza kuniongelea vibaya mitandaoni baada ya kikosi kutolewa kwani wengi waliamini ningepata kadi nyekundu au kutoa penalti ila imekuwa tofauti.
“Matokeo kwa upande wangu yameniumiza licha kwamba sijacheza vizuri kwenye kiwango changu kwa sababu hatujafungwa katika mechi 11 halafu tunakuja kuharibu rekodi katika mchezo ambao kwangu ni wa kwanza kucheza kwenye, ligi inaumiza,” alisema Ninja.
No comments:
Post a Comment