Saturday, January 13, 2018
SEVEN DAYS IN HELL (SIKU SABA KUZIMU)- 48
ILIPOISHIA:
“Nakupenda Jamal,” alisema kisha akanibusu kwenye shavu langu la upande wa kushoto, mwili wote ukasisimka tena, nikakosa hata cha kujibu zaidi ya mimi kumkumbatia pia na kumbusu, uvuguvugu wa joto la mwili wake ukanifanya nitamani niendelee kumkumbatia lakini nilipokumbuka mtihani mzito uliokuwa mbele yangu, nilimuachia, nikatoka haraka na kwenda kumuamsha Raya, harakaharaka tukaanza kujiandaa.
SASA ENDELEA…
Muda mfupi baadaye, tayari tulikuwa tumeshamaliza kujiandaa, mimi na Raya tukasaidiana kumbeba Shenaiza ambaye bado alikuwa haelewi chochote kinachoendelea, Firyaal akaenda kuwasha gari. Ilibidi kila kitu kifanyike harakaharaka kama Shamila alivyotuambia.
Kwa bahati nzuri tulifanikiwa kutoka salama, tukafunga milango yote na kuiacha funguo mahali alipokuwa ametuelekeza Shamila. Kwa kuwa bado ilikuwa ni asubuhi, hakukuwa na foleni sana barabarani, safari ya kuelekea Kimara Temboni ikaanza.
Ilibidi nimuombe Raya simu yake kwa ajili ya kumpigia yule mtu ambaye Shamila aliniambia kwamba ni ndugu yake ambaye ndiye angeenda kutupokea na kutupa hifadhi. Namshukuru Mungu kwamba nilivyopiga mara moja tu, alipokea, tukazungumza na kuelewana.
Nikawa namuelekeza Firyaal kama na mimi nilivyoelekezwa na yule mwenyeji wetu, kwa bahati nzuri tulipofika Kimara Temboni tu, mwanamke wa makamo, mweupe na mnene kiasi, alitupokea. Yeye alikuwa amepanda bodaboda, akatonesha ishara kwamba tumfuate, Firyaal ambaye alikuwa na uzoefu wa kutosha wa kuendesha gari, akawa anamfuata.
Tulishuka makorongo mpaka tulipotokea ng’ambo ya pili, akasimama mbele ya geti kubwa jeusi na kumlipa yule dereva wa bodaboda, akasubiri mpaka aondoke kisha ndiyo akatufuata. Kwa kuwa kiumri alikua mkubwa kwetu, sote tulimuamkia kwa heshima, akamwambia Firyaal inabidi aliingize gari ndani ya geti kwa usalama zaidi.
Akatufungulia geti na muda mfupi baadaye, tayari tulikuwa ndani, tukasaidiana kumshusha Shenaiza mpaka ndani, akatukaribisha na kututaka kuwa makini kwa muda wote ambao tutakuwa pale nyumbani kwake.
“Inaonesha mambo siyo mazuri kwa Shamila, nimetoka kuongea naye sasa hivi na yeye ndiye mtuhumiwa namba moja, lazima atapewa kashikashi kubwa na polisi kwa hiyo inabidi sote tutulie tusije tukasababisha matatizo mengine, kuweni makini sana na simu zenu,” alisema, wote tukatingisha vichwa kama ishara ya kumuelewa.
Kwa kuwa nyumba ilikuwa kubwa, alitupangia kila mmoja chumba chake na kutuambia tutakaa hapo mpaka mambo yatakapotulia. Ilionesha kwamba mwanamke yule anajimudu sana kimaisha kwa jinsi mazingira ya pale nyumbani kwake yalivyokuwa.
Muda ulizidi kuyoyoma huku nikiwa na shauku kubwa ya kutaka kujua nini kitatokea kwa Shamila kwani kama ni matatizo, basi tulikuwa tumemsababishia makubwa sana.
“Kuna anayejua kufanya ‘meditation’ kati yenu?” aliuliza mwanamke huyo ambaye baadaye alituambia kuwa tuwe tunamuita mama wawili, wote tukatazamana.
“Shamila yupo kwenye matatizo makubwa, inatakiwa tufanye kitu kumuokoa vinginevyo mambo yatakuwa mabaya sana kwake,” alisema, nikashindwa kuelewa uhusiano uliokuwepo kati ya kufanya meditation na kila alichokuwa anakizungumza.
“Kwani meditation ni nini?” nilimuuliza nikiwa na shauku kubwa, akanitazama bila kunijibu chochote kwa sekunde kadhaa kisha atatuambia mimi, Raya na Firyaal tumfuate, tukaingia ndani ya chumba kimoja kilichokuwa kimetandikwa zulia jekundu la bei mbaya.
“Hata kama hamjui ni lazima tushirikiane kumsaidia Shamila, mimi peke yangu siwezi, nitawafundisha nini cha kufanya,” alisema, sote tukashusha pumzi ndefu na kuanza kumsikiliza. Akatuambia kwamba kwa kawaida, binadamu tuna nguvu kubwa zisizoonekaa kwa macho, ambazo kama zikitumiwa vizuri zinaweza kutoa matokeo makubwa.
Akasema jukumu la kwanza ambalo tulitakiwa kulifanya kwa muda huo, ilikuwa ni kumkomboa Shamila kutoka kwenye mkono wa sheria, sikumuelewa kabisa alichokuwa anamaanisha, ikabidi nimuulize.
Akaniambia kwamba tunatakiwa wote tukae na kutulia katika mkao ambao kila mmoja wetu ataruhusu nguvu aliyonayo itumike kwa ajili ya kazi iliyokuwa mbele yetu, bado sikumuelewa zaidi ya kuona kama ananichanganya kichwa.
“Kuna kitu kinaitwa out of body experience au kwa kifupi OBE, yaani mwili wako unakuwa upo hapa lakini kwa wakati huohuo unakuwa sehemu nyingine tofauti ukifanya kitu kingine tofauti kabisa,” alizidi kutueleza lakini bado kwangu ulikuwa ni sawa na usiku wa giza.
Hamjawahi kusikia au kuona mtu anajitazama mwili wake mwenyewe akiwa nje ya mwili huo?” alisema kitu ambacho kiliushtua sana moyo wangu, mapigo ya moyo yakaanza kunienda mbio. Kilichofanya nishtuke ni kwamba kile alichokuwa akikizungumza, mimi kilishawahi kunitokea lakini nilikuwa sijui ni nini na inakuwaje.
Nilikumbuka vizuri siku nilipovamiwa na wale watu ambao walinishambulia vibaya na kutaka kuyakatisha maisha yangu, muda huohuo nikaanza kuhisi kama napaa halafu nikawa nauona mwili wangu ukiwa umelala chini, damu nyingi zikitoka kwenye jeraha la kifuani.
Nilikumbuka kila kitu ambacho kiliendelea kutokea na maruweruwe yote mpaka siku nilipokuja kuzinduka na kurejewa na fahamu zangu.
“Mbona kama uko mbali kimawazo? Tunaenda pamoja kweli?” alihoji mama wawili huku akiwa amenikodolea macho, nikawa namtazama lakini akili zangu zipo kwenye ulimwengu mwingine kabisa, ni kama alijua kwani alinishika na kusababisha nishtuke sana, wote wakawa wananishangaa.
“Ili hiki tunachoenda kukifanya kitimie lazima kila mmoja akili zake ziwe hapa, umenisikia kaka?” alisema mama wawili akinilenga mimi, nikashusha pumzi ndefu na kukaa vizuri. Akaendelea:
“Sasa kwa kuwa kati yenu hakuna anayejua tunachoenda kukifanya, nawaomba kila mmoja atulie tukiwa tumeshikana kisha mimi nitazitumia nguvu zenu kufanikisha hili linalotukabili, mambo mengine tutaendelea kuelekezana taratibu, tumeelewana?” alisema, wote tukaitikia kwamba tumemuelewa.
Akatuelekeza namna ya kukaa, wote tukakunja miguu na kuzunguka kama duara, akatuambia kila mmoja anatakiwa afumbe macho, ainue shingo yake na kupumua kwa uhuru kabisa huku akitutaka kutuliza akili zetu sehemu moja.
“Unatulizaje akili sehemu moja?”
“Nyie wote si mnaijua vizuri hospitali anayofanya kazi Shamila si ndiyo?”
“Ndiyo.”
“Basi nataka mkifumba macho, kila mmoja avute picha na kuanza kujiona kama yupo pale hospitalini na mtulize akili hapohapo, tumeelewana?” alisema mama wawili, wote tukatii alichotuambia, tukaweka duara na kushikana mikono, kila mmoja akawa anavuta hewa na kuitolea mdomoni kama alivyotufundisha.
Ndani ya dakika mbili tangu tukae mkao huo, kuna mambo ya ajabu yalianza kunitokea, mapigo ya moyo yakawa yanazidi kwenda mbio kuliko kawaida kutokana na kile nilichokuwa nakishuhudia.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment