Thursday, January 4, 2018

Agizo la kukamatwa kwa Wazazi na wanafunzi wajawazito latekelezwa


Mtwara. Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara,  Sebastian Waryoba amesema agizo lake la  kuwakamata wazazi na wanafunzi 55 wa sekondari waliopata ujauzito hata kama walishaacha shule miaka miwili iliyopita,  limeanza kutekelezwa na mpaka sasa amekamatwa mtu mmoja.

Akizungumza leo  Alhamisi Januari 4, Waryoba amesema changamoto wanayokabiliana nayo kwa sasa ni wahusika kukimbia.

Waryoba alitoa agizo hilo Desemba mwaka jana katika kikao cha kamati ya ushauri ya wilaya baada ya kupokea taarifa ya elimu kutoka kwa Ofisa Elimu Sekondari, Sostenes Luhende kuhusu wanafunzi hao kupata ujauzito kati ya Januari na Desemba.

“Zoezi linakwenda vizuri na tumefanikiwa kumkamata mtu mmoja,  baadhi yao baada ya kusikia msako huu unaondelea wamekimbia. Hii ndio changamoto ambayo tunaipata,” amesema,

“Lakini jitihada mbalimbali zinaendelea  kuhakikisha wahusika wote wanafikishwa katika mikono wa sheria,” amesema Waryoba.

Amesema baada ya wahusika kukamatwa, watawekwa hadharani ili wananchi waweze kuwaona lengo likiwa ni kuonyesha kuwa agizo hilo halikuwa la mzaha.

Mimba kwa wanafunzi wa kike wa shule za sekondari wilayani Tandahimba bado ni changamoto, taarifa zinaeleza kuwa wanafunzi 20 walipata ujauzito mwaka 2015, mwaka 2016 wanafunzi 27 na mwaka jana 55.


No comments:

Post a Comment