Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(Takukuru) mkoani Kilimanjaro inamshikilia karani wa Mahakama ya Mwanzo ya Maili Sita wilayani Hai, Rose Urassa (58) kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa ya shilingi laki moja.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Kilimanjaro, Holle Makungu amesema karani huyo aliomba fedha hiyo kwa madai ya kumsaidia mshitakiwa katika kesi ya jinai namba 69/2017 kupitia kwa hakimu anayesikiliza kesi hiyo aweze kutoa hukumu yenye upendeleo kwa mshitakiwa.
Mtuhumiwa huyo alikamatwa jana Jumatano Januari 3 katika eneo la mahakama hiyo akiwa amepokea fedha hizo baada ya taarifa hizo kupokelewa na ofisi ya Takukuru na mtego wa rushwa kuandaliwa katika eneo hilo.
Mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani mara baada ya uchunguzi Kukamilika.
Makungu ametoa rai kwa baadhi ya makarani wa wahudumu wa Mahakama wanaoendekeza tabia ya kuomba na kupokea rushwa kwa kisingizio cha kutumwa na mahakimu kubadili tabia hiyo.
Amesema wale watakaoendelea na tabia hiyo wakikamatwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao na kwamba mwaka 2018 utakuwa mwisho wao wa utumishi wa umma.
No comments:
Post a Comment