Saturday, January 13, 2018
SEVEN DAYS IN HELL (SIKU SABA KUZIMU)- 50
ILIPOISHIA:
“Ndiyo,” nilisema kwa kujiamini, akanitazama usoni kisha akaenda mlangoni na kufungua, akawaita Raya na Firyaal, wakaingia ndani na tukakaa tena kama tulivyokuwa tumekaa mwanzo, kazi ikaanza upya huku akinisisitiza kuwa makini na kuishinda hofu ndani ya moyo wangu, nikatingisha kichwa kama ishara ya kukubaliana naye.
SASA ENDELEA…
Kazi ilianza upya, akatusisitiza kila mmoja awe anavuta pumzi ndefu kwa kutumia tumbo na siyo kifua kama wengi tunavyopumua, pia akatutaka kuhakikisha kila mmoja akili yake aielekeza eneo la tukio.
Muda mfupi baadaye, ile hali ilianza kunitokea tena, nikawa najihisi kama naelea angani huku mwili mwingine ukiwa palepale tulipokuwa tumekaa. Hofu ilianza kunijia tena lakini nilipokumbuka maneno ya yule mwanamke, nilijitahidi kuishinda hofu.
Nikaendelea kutuliza kichwa na kufumba na kufumbua, nilijikuta nikiwa pale hospitalini nilipokuwa nimelazwa. Niliweza kuona kila kitu kilichokuwa kikiendelea, wagonjwa waliokuwa wakiingia na kutoka, manesi na madaktari waliokuwa wakikimbizana huku na kule kuelekea kwenye ukumbi wa mikutano.
Upande wa Kaskazini kulikuwa na magari matatu ya polisi yaliyokuwa yamepaki huku askari wengi wenye silaha wakirandaranda huku na kule.
“Kumetokea nini kwani leo hapa?”
“Nasikia kuna wagonjwa wametoroshwa usiku sasa ndiyo polisi wamekuja kutafuta wahusika.”
“Mh! Yaani wagonjwa kutoroshwa tu ndiyo zije difenda kibao na askari utafikiri kuna vita?”
“Nasikia huyo mgonjwa mmoja ni mtoto wa kigogo mmoja mkubwa ndiyo maana unaona hali ipo hivi,” niliwasikia watu wawili wakihojiana, wakiwa wamesimama chini ya kivuli cha mti.
Ghafla nikasikia vishindo vya mtu akitembea kwa kasi nyuma yangu, nikageuka, katika mazingira ambayo sikutegemea, nilimuona askari mmoja mwenye bunduki, akiwa ananifuata pale nilipokuwa nimesimama, nikajua ameshaniona na kunitambua, nikawa natetemeka.
Cha ajabu, ni kwamba alinipita akiwa ni kama hajaniona na kuwafuata wale watu waliokuwa wakiendelea na majadiliano pale chini ya mti, nikamsikia akiwapa amri kwamba hatakiwi mtu yeyote asiyekuwa na shughuli maalum kuonekana ndani ya hospitali hiyo, akawataka watoke nje ya geti na kwenda nje kabisa.
Kidogo nilishusha pumzi kwani nilikumbuka mara nyingi ninapokuwa kwenye hali kama ile, huwa siwezi kuonekana kwa macho ya kawaida. Harakaharaka nikawa nawafuata wale manesi na madaktari kule walikokuwa wanaelekea kwa lengo la kwenda kuona kinachojadiliwa.
Cha ajabu zaidi, nilipofika kwenye mlango wa kuingilia kwenye ule ukumbi, nilimkuta yule mwanamke, mama yake mdogo Shamila naye akiwa ameshafika, nikamtazama nikiamini yeye hawezi kuniona. Cha ajabu na yeye aligeuka haraka na kunikazia macho, tukawa tunatazamana.
Nilijifunza kitu kingine kwamba kumbe ukiwa katika hali ambayo huwezi kuonekana kwa macho ya kawaida, akija mtu mwingine ambaye naye anakuwa kwenye hali kama yako, mnaweza kuonana vizuri, yaani yeye akakuona na wewe ukamuona ingawa watu wengine wa pembeni wanakua hawana uwezo wa kumuona yeyote kati yenu.
Alinisogelea na kunigusa, kingine cha ajabu ni kwamba nilihisi kabisa kwamba nimeguswa na mtu, akanivutia pembeni na kuanza kuzungumza na mimi kwa sauti ya chini, akaniambia Shamila yuko ndani na amewekwa chini ya ulinzi, amejaribu kumtorosha lakini ameshindwa peke yake, akaniomba tukaunganishe nguvu ili tumtoe haraka iwezekanavyo.
“Sasa tutafanyaje” nilimuuliza huku hofu ikianza kuniingia kwani kwa mbali niliwaona askari wengine wawili wenye silaha wakija, akaniambia tukiingia niwe namfuatisha kila anachokifanya, nikatingisha kichwa kuonesha kukubaliana naye. Akaniminya mkono na kunitazama usoni, akaniambia natakiwa niishinde hofu ndani ya moyo wangu. Nadhani aliniona jinsi nilivyoanza kuingiwa na wasiwasi, nikatingisha tena kichwa.
Pale kwenye geti la kuingilia, alinionesha ishara kwamba tunatakiwa kuingia kinyumenyume, tukafanya hivyo na muda mfupi baadaye tayari tulikuwa ndani. Madaktari na manesi walikuwa tayari wameshakaa kwenye nafasi zao huku wengine wakiendelea kuingia.
Mbele kabisa kulikuwa na meza kuu ambako walikuwa wamekaa watu walioonesha kuwa viongozi wa juu wa hospitali hiyo pamoja na askari aliyekuwa na nyota nyingi mabegani, nadhani alikuwa ni kiongozi wa polisi.
Upande wa kushoto, alikuwa amekaa Shamila huku amezungukwa na askari wawili wa kike, mmoja kila upande. Pembeni kidogo, walikuwa wamekaa wale walinzi tuliowapita getini usiku wakati tukitoroka, ambao nao ilionesha wamewekwa chini ya ulinzi. Tulipita mpaka mbele kabisa huku mtu yeyote akiwa hatuoni.
Akanipa ishara kwamba tunatakiwa kuwazunguka wale askari waliokuwa wamemuweka chini ya ulinzi Shamila mara saba kwa uelekeo tofauti, yaani mimi nianzie kulia kwenda kushoto na yeye kushoto kwenda kulia.
Tulianza kufanya kazi hiyo huku kukiwa hakuna mtu yeyote aliyekuwa akielewa kinachoendelea. Tulizunguka mzunguko wa kwanza, wa pili na hatimaye mizunguko saba ilitimia, akanionesha ishara kwamba inatakiwa tuwaguse vichwani wale askari, kweli tulifanya hivyo.
Katika hali ambayo sikuitegemea, nilishangaa kuwaona wale askari wawili wa kike, wote wakishikwa na usingizi wa ghafla, Shamila naye akawageukia mmoja baada ya mwingine, akashangaa akiwa haelewi chochote kinachoendelea.
Wakati hayo yakiendelea, pale meza kuu daktari mmoja alikuwa akizungumza kwa kutumia kipaza sauti, akielezea jinsi tukio la kutoroshwa wagonjwa wawili lilivyofanyika usiku.
Hatukuwa na muda wa kupoteza, alionesha ishara kwamba tukamshike Shamila, mmoja kwenye bega la kushoto na mwingine bega la kulia, tukafanya hivyo kisha akanionesha ishara kwamba akihesabu mpaka tatu, tupige mguu wa kushoto chini kwa nguvu na kufumba macho na nisifumbue mpaka atakaponiambia.
Akaanza kuhesabu, moja! Mbili! Taaatu, nikakanyaga mguu wangu wa kushoto chini kwa nguvu, sawasawa na yeye, mara umeme ukakatika jengo zima, nikafumba macho kama alivyoniambia huku nikiwa nimemshikilia Shamila kwa nguvu, nikahisi kama tumezolewa na kimbunga chenye nguvu kubwa.
“Fumbua macho,” alisema, nilipofumbua macho, sikuamini nilichokiona. Tulikuwa tumerejea ndani ya kile chumba tulichokuwemo mwanzo lakini tofauti na awali, safari hii kila mmoja alikuwa amelala sakafuni, kuanzia mimi, yule mwanamke, Raya na Firyaal huku akiwa ameongezeka mtu mwingine kati yetu, Shamila.
Bado wale wenzetu wote walikuwa kama wamepitiwa na usingizi mzito isipokuwa mimi na yule mwanamke pekee, nikajivutavuta na kuinuka pale nilipokuwa nimelala, nikashangaa mwili wangu ukiwa umechoka kupita kiasi huku viungo vyote vikiniuma.
Yule mwanamke naye aliinuka na kukaa kwa kujiegemeza ukutani, naye akionesha kuchoka kuliko kawaida.
“Kweli wewe ni mwanaume wa shoka, njoo nikupongeze,” alisema kwa sauti ya kichovu, nikajikokota na kusimama, nikasogea mpaka pale alipokuwa amekaa, akanionesha ishara kwamba nikae chini pembeni yake, nikafanya hivyo huku sote macho yetu yakiwa kwa Shamila.
“Sikuwahi kudhani kwamba unaweza kuwa na nguvu kubwa kiasi hicho, hongera sana, utanifaa sana wewe,” alisema huku akipitisha mkono wake mmoja begani kwangu kichovu kisha akanigeukia, tukawa tunatazamana. Katika hali ambayo sikuitegemea hata kidogo, nilishangaa yule mwanamke akinibusu, tena mdomoni, nikashtuka mno.
“Hongera sana, ila inabidi upunguze mambo ya wanawake, utakuwa na nguvu zaidi ya hizi ulizonazo,” aliniambia huku akinitazama usoni.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue au bofya Simulizi za Majonzi kusoma mwendelezo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment