Wednesday, January 3, 2018

TFF yaamua kushirikiana na TAKUKURU



Raisi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania(TFF)  Wallace Karia ameweka wazi kuwa wanashirikiana na TAKUKURU kushughulikia vitendo vya hujuma, uonevu na upendeleo uliojitokeza kwenye mechi mbili za ligi daraja la kwanza.

Karia ametoa kauli hiyo leo ikiwa ni siku moja tu baada ya Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe kulitaka shirikisho hilo kushughulikia haraka malalamiko ya vilabu hivyo.

''Tunashirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) ili kudhibiti vitendo visivyo vya kiungwana michezoni ukiwemo utata uliojitokeza katika mechi hizo mbili, na Taasisi hiyo tutawapatia ratiba ya mechi zote ili iweze kufuatilia kwa ukaribu'', amesema Karia.

Rais Karia amesema tayari wameshaanza kuyafanyia kazi malalamiko yanayohusu michezo iliyohusisha Dodoma FC ya Dodoma dhidi ya Alliance ya Mwanza na Biashara Mara dhidi ya Pamba ya Mwanza ambapo utaratibu utafuatwa na yeyote atakayebainika kutenda hujuma hatua kali dhidi yake zitachukuliwa.

Sio mara ya kwanza kwa ligi daraja la kwanza nchini kukumbwa na migogoro ambapo msimu wa 2015/16 ulitokea utata kwenye mechi za mwisho za kuamua nani apande ligi kuu hali iliyopelekea timu za Geita Gold Mine, JKT Oljoro FC, JKT Kanembwa na Polisi Tabora kushushwa daraja na nafasi ya kupanda daraja kupewa Mbao FC ya Mwanza.

Michezo ya Dodoma FC dhidi ya Alliance na Biashara dhidi ya Pamba ilichezwa Disemba 30 na maamuzi yake kugubikwa na utata mkubwa kabla ya viongozi wa vilabu hivyo kuwasilisha malalamiko yao kwa Waziri Mwakyembe ambaye alimwagiza Rais wa TFF Wallace Karia na viongozi wengine wahusika kuchukua hatua haraka.

No comments:

Post a Comment