Uongozi wa Kiwanda cha Urafiki umetangaza kiama kwa wapangaji wake ukiwataka kulipa kodi la sivyo wataondolewa pasipo huruma wala kuangalia hadhi ya mtu.
Akizungumza na Mwananchi leo Januari 4, 2018, naibu meneja mkuu wa kiwanda hicho, Shadrack Nkelebe amesema notisi ya siku 30 waliyotoa kwa wapangaji hao katika nyumba zilizopo Urafiki Kota, Ubungo imekwisha.
Desemba 21 mwaka jana uongozi wa kiwanda hicho ulitangaza kiama kwa wapangaji zaidi ya 160 ukiwataka kulipa kodi la sivyo watawaondoa.
Miongoni mwa walioponea chupuchupu kuondolewa katika nyumba hizo ni meya wa zamani wa Halmashauri ya Kinondoni, Salum Londa aliyelipa Sh18milioni huku mchezaji wa zamani wa Yanga, Zamoyoni Mogella aliyekuwa akidaiwa Sh5milioni, ikielezwa ataondolewa wakati wowote.
“Wiki ijayo tutaanza kuwatoa wapangaji wetu ambao wamekuwa sugu kulipa madeni ya kodi, tumefanya ubinadamu, tumewaita viongozi wa serikali za mitaa ili shughuli ya kuwatoa ikianza wasishangae,” amesema Nkelebe,
“Wapo ambao wameanza kuja kulipa na wapo ambao wameanza kukimbia, hao tutawatafuta, hatutakubali kodi yetu waondoke nayo. Wale ambao mpaka sasa hawajalipa, tunawashauri tu walipe wasije kupata adha ya kutolewa kwa vitu vyao nje.”
Operesheni ya kuwaondoa inafanywa na Kampuni ua Udalali ya Yono ambayo mwezi uliopita uliwaondoa wapangaji wa nyumba hizo wenye ofisi kwa kuchukua vifaa ili kufidia madeni yao, huku baadhi Nkelebe akisema wamekwisha kuanza kulipa.
“Wapo ambao tayari wamelipa na kuchukua vitu vyao lakini wapo ambao hawajafanya hivyo. Tunataka fedha hizo ili ziweze kuingizwa katika shughuli zetu kama za kununua pamba, kulipa wafanyakazi, ukarabati wa majengo na mashine,” amesema Nkelebe.
No comments:
Post a Comment