Mamlaka ya Mapato nchini kupitia kampuni ya Yono Aunction Mart imeendesha mnada wa magari 140 yaliyotelekezwa bandarini.
Licha ya watu wengi kujitokeza kwenye mnada huo uligubikwa na malalamiko huku wateja wakilalamikia utaratibu mbovu wa uendeshaji wa mnada.
Mwananchi ilishuhudia watu waliofika kwa wingi katika eneo hilo wakiondoka huku wengine wakiwa wamekaa chini kwa kukata tamaa.
Wananchi hao walidai kuwa matarajio yao yalikuwa tofauti kabisa na hali waliyoikuta kwenye mnada kwa kile walichodai kuwa bei zilishapangwa.
Mmoja wa wateja hao Posian Simon amesema alitegemea kuwa mnada huo ungekuwa huru na wanunuzi wangeshindana kwa bei lakini inaonekana kuwa bei zimepangwa.
“Nilijua kuwa mwenye pesa kubwa kuliko wenzake ndiye anayechukua gari sasa hapa mambo yako tofauti mnaweza kushindana na ikafika kiwango cha mwisho lakini wenyewe wakaamua gari haliuzwi kwa kuwa haijafikiwa bei wanayotaka,”
“Nimefunga safari kutoka Bukoba kuja kushiriki kwenye mnada huu ila naona nimepoteza muda wangu na kuja kuteseka na jua, nashauri siku nyingine uwekwe utaratibu mzuri”
Malalamiko kama hayo aliyatoa Diwani wa Tabata,Patrick Assenga ambaye pia alifika katika eneo hilo kwa ajili ya kununua gari.
“Kwa kweli kinachoendelea hapa ni kitu cha ajabu, nilijua mnada huu utafuata taratibu za minada mingine ambayo watu wanashindana na anayeshinda ndiye anapaswa kuchukua mali lakini hapa mtu anaweza fikia kiwango cha juu na bado wakaamua gari iwekwe pembeni,
“Kinachonishangaza zaidi ni hizi bei wanazozitaka wao yani ni sawa na mtu akaenda show room kuchukua gari au labda na wao wangebandika bei kwa kila gari maana hakuna haja ya kuwajaza watu kwenye jua hapa halafu wanafanya mambo tofauti na utaratibu,” amesema Assenga.
Akijibu kuhusu malalamiko hayo Mkurugenzi Mtendaji wa Yono Auction Mart, Scolastica Kevela amesema mnada huo unazingatia taratibu zote na watu wanashinda kwa bei kama inavyopaswa kuwa.
Kuhusu kusitisha uuzaji wa baadhi ya magari licha ya kuwa kuna kiwango cha bei kilichofikiwa Kevela amesema mauzo yoyote yanafikiwa kulingana na thamani ya gari husika.
“Hata kama Serikali inataka kukomboa kodi yake haiwezekani bei kuuzwa kwa bei ya kutupa, lazima tuzingatie thamani halisi ya gari. Kwa kifupi mambo yanakwenda vizuri kabisa,”
No comments:
Post a Comment