Wednesday, January 3, 2018

Nafasi ya Mtulia na Mollel kuzibwa Februari 17




Uchaguzi mdogo wa ubunge katika majimbo ya Siha mkoani  Kilimanjaro na Kinondoni, Dar es Salaam pamoja na kata nne za Tanzania Bara utafanyika Februari 17,2018.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), katika taarifa iliyotolewa leo Januari 3,2018 imesema uchaguzi unafanyika kutokana na waliokuwa wabunge katika majimbo hayo kujivua uanachama na kukosa sifa za kuendelea kuwa wabunge.

Waliokuwa wabunge katika majimbo hayo ni Maulid Mtulia wa Kinondoni kupitia CUF na aliyekuwa Siha, Dk Godwin Mollel walijivua uanachama na kujiunga na CCM.

Taarifa ya Makamu Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mkuu mstaafu wa Zanzibar, Hamid Mahmod Hamid imesema kata nne zitakazofanya uchaguzi ni za Isamilo iliyopo Halmashauri ya Wilaya  ya  Nyamagana mkoani  Mwanza.

Nyingine ni Manzase katika Halmashauri ya Wilaya  ya Chamwino mkoani Dodoma; Madanga katika Halmashauri ya Wilaya ya Pangani mkoani Tanga;  na Kimagai katika Halmashauri ya Wilaya ya  Mpwapwa mkoani Dodoma.

Amesema Tume inaendesha uchaguzi baada ya kupokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge, Job  Ndugai kuhusu majimbo hayo kuwa wazi.

Jaji Mahmoud amesema barua hiyo ilieleza kuwa  majimbo hayo yapo wazi baada Mtulia na Dk Mollel kujiuzulu uanachama wa vyama vyao hivyo kukosa  sifa za kuwa wabunge.

Pia, amesema Tume ilipokea taarifa kutoka kwa  Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa  ikiitaarifu uwepo wa nafasi wazi za udiwani katika  kata nne za Tanzania Bara.

“Baada ya kupokea barua hizo Tume kwa kuzingatia  vifungu vya 37(1) na 46(2) vya Sheria ya Taifa ya  Uchaguzi sura ya 343 pamoja na  kifungu cha 13(3)  cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa sura ya  292 inatangaza kuwa majimbo mawili na kata nne  zipo wazi” amesema.

Amesema fomu za uteuzi kwa majimbo hayo  mawili na kata nne itakuwa kati ya Januari 14 na 20,2018.

Makamu mwenyekiti huyo wa NEC amesema   uteuzi wa wagombea utafanyika Januari 20,2018 na kampeni za uchaguzi mdogo zitafanyika kuanzia  Januari 21 hadi Februari 16, 2018 na siku ya  uchaguzi itakuwa  tarehe Februari 17,2018.

Amevikumbusha vyama vya siasa na wadau wote  wa uchaguzi kuzingatia sheria, kanuni, utaratibu,  miongozo na maelekezo yote wakati wa uchaguzi  huo mdogo.


No comments:

Post a Comment