Friday, January 5, 2018

Marubani wa kike wapigana makonde angani


MARUBANI WA KIKE WA JET AIRWAYS.

MARUBANI wa shirika la Jet Airways la India, siku ya mwaka mpya walifanya vituko vya ajabu angani kwa kuchapana.

Ugomvi huo ulitokea angani, baina ya rubani wanawake wa ndege inayosafiri kati ya jiji la London, Uingereza na Mumbai, India, rubani mkuu alipomchapa kibao msaidizi wake.

Hata hivyo inaelezwa, licha ya kuwa msaidizi, rubani huyo pia ni mwandamizi kwa maana ya kwamba, amesafiri angani kwa saa nyingi, hivyo anaimudu vyema kazi hiyo.

Inaelezwa, tukio lilijulikana baada ya rubani aliyepigwa, kutoka nje ya chumba chao kwenye ndege akigugumia kwa machozi ya hasira.

Kutokana na tukio hilo, Mamlaka inayosimamia anga nchini India, limewasimamisha kuendesha ndege, kuchunguza kisa cha kutokea mkasa huo wa aina yake.

Wakati tukio linatokea, ndege ilikuwa na abiria 324 na ilisikika sauti ya kipaza sauti cha rubani ikimwita aliyepigwa.Baadaye, rubani mkuu aliyeongea kwenye kipaza sauti, alilazimika kutoka kumbembeleza mwenzake arudi chumbani kwao, akakubali. Lakini, ghafla alirudi tena nje akionyesha hali ya hasira.

Katika hatua hiyo ya pili, watumishi wa ndege walilazimika kwenda kumbembeleza mwenzao akarejea ndani.

Taratibu za ndege za India, ni kwamba chumba cha rubani kinakuwa na walau rubani wawili.Sakata hilo limemgusa sana mwajiri wao shirika la Jet, aliyeanzisha uchunguzi mkali kupata undani wa suala hilo, huku walalamikwa wakichunguzwa.

Mamlaka ya usfairi wa anga nchini India imeagiza uchunguzi mkali, wakati huohuo imesimamisha leseni za marubani hao wawili kinamama, ikisubiri matokeo ya uchunguzi.



No comments:

Post a Comment