WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, (UTUMISHI NA UTAWALA BORA, GEORGE MKUCHIKA.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na ofisi zote za maadili zimeagizwa kuhakikisha viongozi hawafanyi biashara na ofisi za umma.
Agizo hilo limetolewa jana na Waziri wa Nchi, ofisi ya Rais, (Utumishi na Utawala Bora, George Mkuchika, alipokuwa akikabidhi fomu ya tamko la rasilimali na madeni kwa viongozi wa utumishi wa umma katika ofisi za maadili Kanda ya Kusini mkoani hapa.
Alisema wizara yake imekuwa ikipokea taarifa kwamba wapo madiwani, wabunge na wakuu wa mashirika ya umma kufanya biashara na halmashauri zao, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.
Sheria ya maadili imekuwa ikizungumzia suala la mgongano wa maslahi ambapo viongozi kumiliki kampuni ambayo imeandikishwa kwa jina la mtu mwingine au kuwa na kampuni ambayo wana hisa, ni kinyume cha sheria.
Kadhalika, sheria inawazuia viongozi hao kukaa kwenye vikao na kuamua mtu wa kupewa zabuni kwa kuwa ni ukiukwaji wa maadili ya utumishi wa umma.
“Wewe mheshimiwa diwani, kuwa na kampuni yako ambayo umeandikisha jina la mtu mwingine au kuwa na kampuni yako ambayo wewe una hisa, lakini na wakati huo huo unakaa kwenye kikoa na kuamua nani apewe tenda katika halmashauri yako hilo ni kosa kwa mujibu wa maadili,” alisema Mkuchika.
Hata hivyo, Mkuchika alielezwa kuwa ofisi hiyo inakabliwa na changamoto mbalimbali za kiutendaji ikiwamo vitendea kazi na rasilimali fedha, hali inayosababisha kushindwa kuwafikia viongozi wa umma na kumuomba na kukuomba azifanyie kazi.
Katibu Msaidizi katika ofisi hiyo, Mayina Henjewele, alisema kuwa, changamoto hizo zimekuwa zikikwamisha utendaji wa kazi zao.
Waziri Mkuchika aliwaahidi na kuwahakikishia watumishi wa ofisi hiyo kuwa atazifanyia kazi changomoto hizo.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Stesheni wilayani Nachingwea mkoani Lindi, Paulina Mchopa, wakati akirejesha fomu hizo alitoa wito kwa madiwani wenzake nchini kutojihusisha na vitendo hiyo, badala yake wawe watetezi wa wananchi.
No comments:
Post a Comment