Friday, January 5, 2018

Babu Seya, Papii Kocha kurekodi wimbo Wanene



Wasanii Wakongwe Nchini, Nguza Viking aka Babu Seya na mwanaye, Johnson Nguza ' Papii Kocha' wakiambatana na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza walitembelea studio za Wanene Entertainment zilizopo Mwenge, Dar es Salaaam.

Wasanii hao walipelekwa katika studio hizo na Waziri Shonza na kupokelewa na mmiliki wa Wanene, Dash ambapo walifanya mazungumzo ya pamoja yaliyolenga kurekodi nyimbo kwa wasanii hao na kusaidiwa kurudisha vipaji vyao ikiwa ni sapoti ambayo Wizara imeamua kuitoa kwa wasanii hao.

Akizungumza na wandishi wa Habari, Naibu Waziri Shonza alisema wao kama Wizara ambayo ina dhamana na tasnia ya muziki imeamua kwa dhati kuwasaidia wasanii hao ambao walipata msamaha wa Rais Desemba 9 mwaka Jana kutokana na kukabiliwa na kifungo cha Maisha jela.

" Sisi kama Wizara tumeamua kuendeleza vipaji vya Wasanii hawa ambao sisi ndio walezi wao, hivyo nimewasiliana na uongozi wa Wanene ambao wamekubali kushirikiana na sisi lengo ni kuhakikisha ubora wa hawa wasanii unarejea na wanafanya kazi" Alisema Shonza.

Nae Mmiliki wa Wanene, Dash alisema wameamua kwa dhati kuwasaidia wasanii hao na kwamba leo wamewaonesha mazingira ya Studio na wakuwasikilizisha baadhi ya midundo ambayo imetengenezwa katika studio zao ili kuwazoesha aina ya muziki ambao upo hivi sasa.

Kwa upande wake Nguza Viking ' Babu Seya aliishukuru Serikali kupitia kwa Naibu Waziri na kuahidi kufanya kazi kama ambavyo Sera ya Rais Magufuli ya hapa Kazi Tu inavyosema na huku akijitamba kurudisha imani ya mashabiki wa muziki wa Dansi.

" Kwa sasa hatuwezi kusema tutarekodi ngoma ngapi lakini tunamshukuru Waziri na Dash kwa sapoti yao, sisi tunachowaahidi ni kufanya kazi kwa bidii kama Rais anavyotaka.

" Mimi ni msanii naweza kufanya aina yoyote ya muziki haijalishi ni wa aina gani, hivyo mashabiki wetu wakae mkao wa kula tumerudi kuwapa burudani," alisema Papii Kocha.

No comments:

Post a Comment