Friday, January 5, 2018

Dk Shein ametaka Muungano ufanyike pia Z'bar



Zanzibar. Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein ametaka jambo linalohusu Muungano linalofanyika Tanzania Bara, lifanyike pia na visiwani humo bila ubaguzi wowote.

Dk Shein ametoa kauli hiyo jana katika ufunguzi wa jengo jipya la Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) liliopo Mazizini nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

Huku akitolea mfano jengo hilo alisema, “Kukamilika kwa jengo hili ambalo linafanana na lile la Dodoma ni ishara mojawapo ya kuwa ipo haja kwa kila jambo la muungano linalofanyika Tanzania Bara na Zanzibar linapaswa kufanyika pia ili kutoufanya upande mmoja kujiona kama umetengwa. Si busara kwa mambo ya muungano kufanywa upande mmoja tu au upande mmoja kuonekana unajivutia wenyewe kila kitu, hali hiyo inaweza kuleta madhara makubwa katika utendaji wa masuala ya muungano.”

Alisema watendaji wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakiwamo mawaziri, naibu mawaziri na watendaji wote wanapaswa kuelewa kuwa mambo ya muungano yasifanywe na upande mmoja.

Alisema jambo hilo likifanyika litasaidia pande zote mbili za Muungano na kusisitiza kuwa ametoa kauli hiyo kwa kuwa ni mzoefu akiwa ametumikia miaka tisa katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

Dk Shein aliishukuru Benki ya Dunia (WB) kwa misaada yake kwa Zanzibar kupitia Serikali ya Muungano, jambo ambalo alisema litarahisisha utaratibu wa ukusanyaji wa takwimu.

Mtakwimu Mkuu wa SMZ, Mayasa Mahfoudh Mwinyi alisema Sh7.9bilioni zimetumika katika ujenzi wa jengo hilo la ghorofa nne lenye vyumba 60 ambalo linatarajiwa kutumiwa na watumishi 164.

No comments:

Post a Comment