Mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongela alikuwepo kwenye mchezo wa Mbao vs Yanga December 31, 2018 kwenye uwanja wa CCM Kirumba mchezo ambao ulimalizika kwa Mbao kuendeleza ubabe kwa Yanga kwenye uwanja huo baada ya kushinda kwa magoli 2-0.
Mongela ambaye ni mdau mkubwa wa michezo hususan soka, baada ya mchezo huo alituma ujumbe kwa shirikisho la soka nchini TFF kwa kuhoji kwamba, tunajifunza nini kutokana na ushindi wa Mbao dhidi ya Yanga mara tatu na kuongeza kuwa, TFF lazima iwe na agenda ya kukuza mpira.
“Tuzilindie heshima Simba, Yanga na Azam lakini TFF lazima iwe na agenda ya kukuza mpira, huon ndio ujumbe wangu ambao nafikiri wakati mwingine Mungu anaamua kutupa ujumbe wowote watanzania. Tusifurahie sana Yanga kufungwa, je tumejifunza nini kutokana na Mbao kuipiga Yanga mara tatu?”-John Mongela.
Ushindi wa Mbao dhidi ya Yanga ulikuwa ni wa tatu mfululizo kwenye uwanja wa CCM Kirumba, timu hizo zimekutana mara tatu kwenye uwanja huo na mara zote Yanga imeambulia kichapo. Yanga imepoteza mechi mbili za ligi kuu Tanzania bara dhidi ya Mbao kwenye uwanja huo na mchezo mwingine ulikuwa wa kombe la shirikisho Tanzania bara (Azam Sports Federation Cup).
No comments:
Post a Comment