Jina la mshambuliaji wa Mbao Habib Kiyombo ameendelea kupata umaarufu na kuwa gumzo kutokana na uwezo wake wa kupasia kamba siku za hivi karibuni.
Kama hujui, Kiyombo amezifunga Simba na Yanga katika mechi za mzunguko wa kwanza msimu huu, alifunga goli lakwanza la kusawazisha kwenye mechi ya Mbao vs Simba iliyomalizika kwa sare ya 2-2 uwanja wa CCM Kirumba ilikuwa September 21 , 2017. Wakati Simba ikiongoza kwa bao 1-0 lililofungwa na Kichuya, Kiyombo alimtungua Manula na kuisawazishia Mbao kufanya matokeo kuwa 1-1.
Jana akafunga magoli yote mawili yaliyoiwezesha Mbao kuibuka na pointi tatu walipocheza dhidi ya Yanga December 31, 2017 kwenye uwanja huohuo wa CCM Kirumba Mwanza.
Kiyombo alifunga magoli matano peke yake wakati Mbao ikishinda 5-1 ugenini dhidi ya Makanyagio ya Katavi kwenye mchezo wa kombe la shirikisho Tanzania bara (Azam Sports Federation Cup) na kuisaidia Mbao kusonga hatua inayofuata.
Ni huyuhuyu Kiyombo ambaye magoli yake mawili ya jana dhidi ya Yanga yamemfanya afikishe jumla ya mabao saba kwenye orodha ya wafungaji bora wa ligi kuu akiwa nyuma kwa goli moja dhidi ya Emanuel Okwi ambaye anaongoza akiwa na magoli nane.
Mwenyewe wala hana maneno mengi: “Nawashukuru wachezaji wenzangu kwa kuonesha ushirikiano mzuri pamoja na mwalimu wangu, kila kisu tunapenda kukaa kama familia, kitu hicho kinanisaidia sana kuweza kufanya vizuri kwa sababu tunakuwa na upendo.”
Kiyombo ni kijana ambaye anakuja juu baada ya kuondoka wakali kama Pius Bwiswita, Salmin Hozza, Jamal Mwambeleko, Benedict Haule, Emanuel Mseja ambao waliifanya Mbao kuwika msimu uliopita kwa kuiwezesha kubaki ligi kuu na kucheza fainali yao ya kwanza ya michuano ya FA Tanzania bara.
No comments:
Post a Comment