Wednesday, January 3, 2018

Rais Magufuli kushusha neema kwa walimu


Rais Dkt. John Pombe Magufuli amesema mwezi ujao Februari ataidhinisha jumla ya kiasi cha Bilioni 200 kulipa madeni mbalimbali yaliyohakikiwa pamoja na madeni ya walimu, makandarasi wa ndani na waliokuwa wakihudumia taasisi za serikali.

Magufuli amesema hayo leo Januari 3, 2018 akiwa Ikulu jijini Dar es Salaam na kusema ataidhinisha pesa hizo ili zitawanywe zikalipe madeni ya wananchi

"Sahizi uchumi unakwenda vizuri sana na bahati nzuri , tuna pesa nyingi nimepanga kwa mfano angalau kuanzia mwezi ujao kwa yale madeni ya ndani wapo watu waliokuwa wanadai, wapo wasambazaji wamesambaza vyakula kwenye mavyuo, kwenye mashule, wapo wakandarasi wamefanya kazi maeneo mbalimbali, wapo wafanyakazi ambao wana madeni yao miaka, walimu yale madeni yote yatakayokuwa yamehakikiwa ilimradi yasiwe madeni hewa mwezi unaokuja nitatoa bilioni 200 ili zikalipe haya madeni" alisema Magufuli

Aidha Rais amesema kuwa angeweza kutoa pesa hizo kwa haraka zaidi hata kesho lakini ameamua kutoa muda mpaka mwezi ujao ili Serikali iweze kufanya uhakiki juu ya madeni hayo na kisha kuwalipa wale wanaostahili kulipwa kutokana na huduma walizofanya kwa serikali.

"Nimeona tuhakiki kwanza haya madeni, process ikikamilika na kumaliza mapema hili suala la uhakiki, ninaruhusu tutoe hizo bilioni 200 ziende kwa wananchi, nina hakika zile zitasaidia wananchi ambao walikuwa waaminifu waliokuwa wakisambaza mahitaji, bilioni 200 si kitu kidogo kukitoa kwa mara moja"

Mbali na hilo Rais Magufuli amesisitiza kuwa fedha hizo zitakazotoka zitumike kulipa madeni ya ndani tu na si madeni ya watu wa nje na kudai kuwa anaamini hiyo ni njia moja wapo ya kukuza uchumi.





No comments:

Post a Comment