Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amesema matendo ya udhalilishaji wa kijinsia kwa watoto yanachangiwa na jamii kuacha kuwalea watoto.
Dk Shein aliyeshiriki bonanza la vikundi vya mazoezi lililofanyika Uwanja wa Amaan mjini Zanzibar amesema udhalilishaji unachangiwa na jamii kutoshiriki malezi.
Amesema leo Jumatatu Januari Mosi, 2018 kuwa jamii inapaswa kutambua mtoto wa mwenzako ni wako, hali iliyosaidia kwa kiasi kikubwa kuwa na malezi bora miaka ya nyuma.
“Zamani mtoto akifanya kosa hutiwa adabu na mtu yeyote, siku hizi hakuna mtu anayethubutu kumtia adabu mtoto wa mwenzake pindi akifanya kosa, hili hutokana na kila mzee kuwa mkali na mwanawe,” amesema.
Dk Shein amesema, “Jambo hili linaonekana kuvipa mwanya vitendo vya udhalilishaji kwa watoto kutokana na jamii kutosaidia katika malezi.”
Amesema Serikali imekuwa ikitafuta njia za kukabiliana na tatizo hilo na imeandaa mkakati wa miaka mitano.
Wakati huohuo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi amesema wananchi wanapaswa kushirikiana na viongozi wa Serikali, taasisi za umma na za kijamii kupiga vita vitendo vya udhalilishaji.
Amesema hayo baada ya kushiriki kazi ya usafi wa mazingira ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.
Kazi hiyo ilifanyika katika majengo ya Hospitali ya Chake Chake kisiwani Pemba.
Amesema udhalilishaji kwa watoto na wazee ni kinyume cha haki za binadamu na hata vitabu vya dini vinakataza.
Alikemea wazazi wenye tabia ya kuwaozesha watoto katika umri mdogo akisema vitendo hivyo vinawanyima haki ya kupata elimu.
No comments:
Post a Comment