Monday, January 1, 2018

Vigogo 180 kitanzini TAKUKURU



TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) inawachunguza wakurugenzi wa halmashauri zaidi ya 180 nchini, kutokana na tuhuma za upigaji wa mabilioni ya shilingi wakidai kutekeleza agizo la Rais kutengeneza maabara kwa ajili ya shule za sekondari.
Upigaji huo mpya ni ulioibuliwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) ukihusisha fedha za miradi ya maendeleo ya miaka ya fedha 2013/14 na 2014/15.
Kamati hiyo ilibaini kuwa agizo la Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete kujengwa maabara kwa kila shule ya sekondari nchini lilitumika kama mwanya wa watendaji hao wa serikali kufuja fedha za umma na kusababishwa kukwama kwa miradi mingi ya maendeleo iliyokuwa imepangwa kutekelezwa 2013/14 na 2014/15.
Hata hivyo, Nipashe inafahamu kwamba kati ya wakurugenzi 185 wa halmashauri za majiji matano, manispaa 21, miji 21 na wilaya 137 kwa upande wa Tanzania Bara walioteuliwa na Rais John Magufuli Julai 7, 2016, ni 65 pekee waliotoka kwenye orodha ya wakurugenzi wa zamani na 120 walikuwa wapya, hivyo baadhi ya wanaochunguzwa hawakalii cheo ukurugenzi kwa sasa.
Akizungumza na Nipashe jijini Dar es Salaam juzi, Ofisa Uhusiano wa Takukuru Makao Makuu, Mussa Misalaba, alisema wako kwenye uchunguzi huo wakifuatilia kwa kina kwa kuangalia maabara zilizojengwa na kiasi cha fedha kilichotumika.
Alisema watakaobainika kutumia agizo la Rais kujinufaisha kwa kufuja fedha za umma watachukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya mwaka 2007.
"Wakati linatokea hili suala mimi nilikuwa Kigoma na ninakumbuka lilileta zogo sana," Misalaba alisema, "'basically' (kimsingi) ni kwamba tumekuwa tukifanya uchunguzi wa suala hili.
"Mimi kipindi kile nilikokuwa (alikuwa Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Kigoma) nilikuwa nimeanzisha uchunguzi kuhusu jambo hili. Na sehemu zingine kuna ufuatiliaji wa namna hiyo.
"Mpaka kufikia sasa sijapata taarifa limefikia wapi maana kuna mafaili mengi, kuna mchanganyiko wa mafaili mengi juu ya suala hili. Kwa kuwa ni suala la kiuchunguzi, nafikiri ni vyema nisiingie ndani sana lakini tunalo, lipo mikononi mwetu linafanyiwa kazi."
Alibainisha kuwa kwa sasa Takukuru ina utaratibu wa kufuatilia kila fungu linalotolewa na serikali kwa ajili ya shughuli na miradi mbalimbali.
"Kwa sasa kila fedha inayotoka tunaifuatilia inapelekwa wapi na inafanya kazi iliyokusudiwa? Je, mradi uliokusudiwa umekamilika? Kwa hiyo, tunafuatilia kwa umakini mkubwa sana. Kuna utaratibu tunaoutumia kwa sasa."
Misalaba aliongeza kuwa mwaka huu wa 2018 wataendelea kukamilisha majukumu ya kipindi kilichopita na kuendelea kutekeleza ambayo yatajitokeza mwaka huu.
AGIZO LA JKNovemba 4, 2012, Kikwete, maarufu JK, aliwaagiza wakuu wa mikoa na wilaya nchini, kujenga maabara kwa kila shule ya sekondari katika kipindi cha miaka miwili kuanzia kipindi hicho.
JK alitoa agizo hilo siku hiyo alipohutubia maelfu ya wananchi wa Jimbo la Manyoni Magharibi mkoani Singida, waliohudhuria mkutano wa hadhara uliofanyika katika mji mdogo wa Itigi.
Alisema maabara ya sayansi ni muhimu katika maendeleo ya wanafunzi kujifunza kwa nadharia na vitendo. JK alisema kutokana na umuhimu huo, kulikuwa kunahitajika ushirikiano kama ule ulioonyeshwa wakati wa ujenzi wa shule za sekondari za kata ulioanza mwaka 2006.
Hata hivyo, Aprili mwaka jana, LAAC ilikosoa utaratibu huo na kufichua ufujaji wa mabilioni ya shilingi uliofanywa na watendaji wa halmashauri na kukwamisha utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo, wakidai pesa zilielekezwa kwenye ujenzi wa maabara.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Vedasto Ngombale, ndiye aliyefichua kadhia hiyo katika mahojiano maalum na Nipashe kwenye viwanja vya Bunge mjini Dodoma Aprili 12, mwaka jana.
Alisema kutokana na tamko hilo la JK, watendaji wa halmashauri walilazimika kuelekeza kwenye ujenzi wa maabara fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya miradi mingine ya maendeleo huku baadhi yao wakipata mwanya wa kufuja fedha za umma kwa kisingizio kwamba wamezielekeza katika utekelezaji wa agizo la Rais.
"Kilichotokea lile lilikuwa tamko, lakini katika maeneo mengi hapakuwa na bajeti kwa ajili ya utekelezaji wa jambo hilo," Ngombale alisema na kufafanua zaidi:
"Kama unavyofahamu, ili kutekeleza mradi wowote katika serikali, sharti kwamba mradi huo utajwe kwenye bajeti, lakini Mheshimiwa Kikwete, kwa mamlaka aliyokuwa nayo, akatoa tamko la utekelezaji wa jambo hilo.
"Sasa, kilichotokea ni kwamba baada ya tamko lile, watendaji wa halmashauri kwa maana ya wakurugenzi watendaji, walichokifanya ni kuchukua pesa kutoka katika kasma mbalimbali kuhakikisha kwamba wanatengeneza maabara.
"Na matokeo yake, tulipokuja kupitia yale mahesabu baada ya utekelezaji, kukawa kumebainika kuna ufujaji mkubwa wa pesa katika halmashauri nyingi."
Ngombale ambaye pia ni Mbunge wa Kilwa Kaskazini (CUF), alisema licha ya tamko hilo kusababisha kutumika kwa mabilioni ya shilingi yaliyokuwa yametengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ikiwamo ya maji, bado kuna halmashauri nyingi hazijakamilisha ujenzi wa maabara, akiitolea mfano halmashauri ya Kilwa anayotoka.
"Zipo halmashauri nyingi ambazo bado hazijakamilisha ujenzi wa maabara hali ya kwamba tamko hilo lilitolewa na utekelezaji ulifanyika kwa kuchukua pesa kutoka katika mafungu tofauti tofauti," alisema Ngombale.
Alisema agizo hilo la JK lilitolewa bila kuwa na bajeti, hivyo fedha za miradi mingine zilikuwa zinachukuliwa na kuingizwa kwenye ujenzi wa maabara, kinyume cha sheria.
"Lakini, katika utekelezaji huo, ndiyo mwanya wa matumizi mabaya ya pesa ulipatikana na sisi tulivyokagua, tumeona ni kiasi gani. Kuna ufisadi mkubwa," alisema.
Alipoulizwa na Nipashe kama upo uwezekano wa wahusika kuchukuliwa hatua za kisheria kupitia Takukuru na pengine kutakiwa kurejesha fedha, Mwenyekiti wa LAAC huyo alisema upo na tayari kamati yake ilishatoa maagizo ilipopitia baadhi ya halmashauri.
KINONDONI BIL. 2.3/-
Alipoulizwa kuhusu halmashauri zilizoongoza kwa utafunaji wa mabilioni hayo, Ngombale alisema: "Kwa ujumla, tatizo hilo lipo katika halmashauri zote nchini na taarifa yetu inaeleza. Mfano, katika ujenzi huo wa maabara Halmashauri ya Kinondoni ilitumia Sh. bilioni 2.281, Urambo Sh. milioni 786.632, Mlele Sh. milioni 725.916, Ngara Sh. milioni 267.143, Rorya Sh. milioni 206.875 na Hai Sh. milioni 200.
"Kumbuka hapakuwa na bajeti ya ujenzi wa maabara na fedha hizo zilitengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mingine ya maendeleo, lakini zikabadilishwa matumizi kinyume cha sheria na watu wakapata mwanya wa kuzipiga."
'Kigogo' huyo wa LAAC alisema mabilioni ya shilingi yaliyotafunwa kupitia mwanya huo yalikuwa yametengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwamo ya maji na barabara.
"Hizi fedha zinatolewa kwa halmashauri kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwamo ya maji na barabara. Zilitumika vibaya sana," Ngombale alisema na kufafanua zaidi:
"Katika kila halmashauri tuliyopitia, tuligundua kuwa zile pesa kwa ajili ya miradi ya maendeleo zilichukuliwa na kuelekezwa kwenye maabara. Pesa hizi ni za mwaka 2013/14 na 2014/15."
Source: Nipashe

No comments:

Post a Comment