WINGA wa kimataifa wa Tanzania, Simon Happygod Msuva anatarajiwa kurejea nchini Alhamisi kwa mapumziko ya baada ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Morocco, maarufu kama Botola.
Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online leo, Msuva amesema kwamba Ligi ya Morocco inakwenda mapumzikoni naye anarejea nyumbani kwa mapumziko na kujipanga kwa mzunguko wa pili.
“Natarajia kurudi nyumbani kuanzia Alhamisi kwa mapumziko ya baada ya mzunguko wa kwanza Ligi Kuu huku, na pia kujipanga kwa mzunguko wa pili kabla ya kurudi kambini,”amesema.
Msuva anaweza kuwa kwenye mapumziko marefu, kwa sababu michuano yote nchini Morocco sasa itasimama kupisha Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) zinazohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee zinazotarajiwa kuanza Januari 13 hadi Februari 4, mwakani.
Simon Msuva (kulia) amefunga mabao matano katika mechi 13 za ligi ya Morocco na ametoa pasi za mabao matatu
Msuva anarejea nyumbani akitoka kuifungia bao pekee Difaa Hassan El-Jadidi ikishinda 1-0 dhidi ya Hassania Agadir Ijumaa.
Msuva, mchezaji wa zamani wa Yanga alifunga bao hilo dakika ya 52 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Ben Ahmed El Abdi mjini El Jadida, Mazghan nchini Morocco na sasa anafikisha mabao matano katika mechi 13 za ligi ya Morocco, akiwa pia ametoa pasi za mabao matatu.
Msuva anazidiwa mabao mawili mawili na Mehdi Naghmi wa Ittihad Tanger na Jalal Doudi wa Hassania Agadir wanaoongoza kwa mabao yao saba kila mmoja, wakifuiatiwa na Mouhcine Lajour wa Raja Casablanca mabao sita sawa na Bilal El Magri, Hamid Ahadad wote wa Difaa Hassan El-Jadidi na Abderrahim Makran.
Mbali na Msuva aliyewahi pia kuchezea Moro United baada ya kupita akademi ya Azam FC, mwingine mwenye mabao matano ni Badr Kachani wa Hassania Agadir.
Ikumbukwe Msuva yupo katika msimu wake wa kwanza Difaa Hassan El-Jadidi baada ya kujiunga na timu hiyo kutoka Yanga SC ya Tanzania.
No comments:
Post a Comment