Sunday, December 31, 2017

Kanisa Katoliki yaitisha maandamano ya amani Kongo



Kuna wasi wasi wa kukosekana utulivu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inayokabiliwa kwa sasa na mgogoro wa kisiasa kufuatia kanisa Katoliki lenye ushawishi mkubwa nchini humo kuitisha maandamano ya amani.

Kabila ambaye waandaaji wa maandamano hayo wanamtaka atamke wazi kuwa hatawania muhula wa tatu wa uongozi, amekuwa madarakani tangu mwaka 2001 wakati aliposhika madaraka ya urais baada ya baba yake Laurent Kabila kuuawa.

Kabila alikataa kujiuzulu bada ya kumalizika  kipindi chake cha pili na cha mwisho  Desemba 2016 hatua iliyosababisha maandamano pamoja na machafuko.

Tangu kipindi hicho maanadamano yamekuwa yakipigwa marufuku licha ya wakati mwingine waandamanaji kukiuka amri ya serikali na kuendelea na maandamano hali ambayo pia imekuwa ikisababisha umwagaji wa damu.

Hatua ya kanisa Katoliki kuitisha maandamano  ya leo Jumapili licha ya serikali kuyazuia yasifanyike inawafanya baadhi ya wachambuzi kuonya juu ya uwezekano wa kukosekana utulivu.

“Maandamano ya leo Jumapili nchini Kongo yanaweza kuwa makubwa zaidi kuliko yale ya mwaka jana” ameandika kupitia ukurasa wa twitter Jason Stearns  mchambuzi aliyebobea katika masuala ya siasa za Kongo kutoka chuo kikuu cha New York kinachohusika na mahusiano ya kimataifa.

Anasema vyama vyote vikubwa vya upinzani, asasi za kiraia, makundi ya vijana wanaharakati pamoja na kanisa Katoliki yanaunga mkono maandamano hayo ya leo Jumapili.

Uchaguzi ulipaswa kufanyika mwaka huu

Uchaguzi ulikuwa ufanyike mwishoni mwa mwaka huu chini ya makubaliano yaliyoasimamiwa na kanisa  katika juhudi za kuzuia machafuko kwenye  taifa hilo kubwa lenye utajiri wa madini ambalo halijawahi kushuhudia mabadilishano ya madaraka kwa njia ya amani tangu lijipazie uhuru wake kutoka Ubeligiji mwaka 1960.

Baada ya kuahilishwa mara kadhaa hasa kutokana na vurugu katika mkoa wa  Kasai  uchaguzi huo uliocheleweshwa sasa umepangwa kufanyika  Desemba 23, mwakani.

Kiasi ya makanisa 150 ya kanisa Katoliki yametoa mwito kwa waumini wao kuitikia wito wa kuandamana  leo Jumapili mjini Kinshasa  wakiwa na biblia mkononi ili kushinikiza kutekelezwa kwa makubaliano yaliyotiwa saini mwaka mmoja uliopita  yaliyokuwa na lengo la  kurejesha uthabiti nchini humo ikiwa ni pamoja na kumtaka Kabila kuondoka madarakani.

Si baraza la maaskofu nchini humo au mwakilishi wa serikali ya mjini Vatican  amezungumzia lolote kuhusiana na maandamano hayo.

Gavana wa mji huo Andre Kimbuta wenye watu milioni 10 amesema jana Jumamosi kuwa maandamano hayo  yasiyo na kibali hayawezi kuendelea kwa maelezo kuwa mji huo hauna maafisa wa polisi wa kutosha kusimamia maandamano  ya leo.

Hata hivyo msemaji wa waratibu wa maandamano  Leonie Kandolo alisisitiza kuwa licha ya kauli hiyo ya serikali maandamano ya leo yatafanyika na kuwa maafisa wa mji huo pamoja na polisi wanalazimika kutimiza wajibu wao kuwalinda raia na mali zao.

Waandaaji wa maanadamano  wametoa mwito kwa waumini kukusanyika baada ya misa ya asubuhi kwa ajili ya kushiriki maandamano leo.

Katiba ya Kongo inamzuia Kabila kuwania muhula wa tatu wa uongozi lakini makubaliano yaliyofikiwa yanamruhusu kusalia madarakani hadi uchaguzi mwingine utakapofanyika.

No comments:

Post a Comment