Sunday, December 31, 2017

Mwaka Mpya wa 2018, Watanzania wakumbushwa kudumisha amani




Katika kuelekea mwaka Mpya wa 2018 watanzania wamekumbushwa kuenzi na kudumisha Mshikamano, Amani na Upendo hususani kwa makundi ya wasiojiweza, yatima na wazee kutokana na kwamba, vitendo hivyo vimeendelea kuwa mhimili na kichocheo muhimu katika kufikia Maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.

Haya yanajidhihirisha kwa vitendo baada ya kikosi cha Jeshi la wananchi 313 Monduli kufika katika kituo cha watoto yatima Global Cha Arusha ambapo kwa pamoja wameshiriki katika shughuli za usafi wa mazingira ya kituo hicho, kufua shuka na mablanket ya watoto lakini pia kutoa msaada wa vitu mbalimbali vyenye thamani ya shilingi milioni Tatu na fedha taslimu shilingi laki tano ikiwa ni ishara ya Upendo kwa yatima hao .

Mkurugenzi wa kituo hicho Mack Donald Kavishe anasema ni kwa mara ya kwanza kupata ugeni kama huo na kuongeza kuwa kitendo cha kushiriki usafi na kutoa msaada huo ni tiba ya kisaikolojia kwa watoto hao ili wasijisikie upweke.

Baadhi ya msaada wa vitu vilivyokabidhiwa ni Sukari, mchele, mafuta ya kujipaka na kupikia, magodoro, chumvi, vifaa vya usafi, madaftari, unga na maharagwe.

No comments:

Post a Comment