Klabu ya soka ya Azam FC leo inatarajia kushuka dimbani dhidi ya Stand United ikisaka alama tatu ili kuizidi Simba SC katika msimamo wa ligi kuu soka Tanzania Bara.
Mchezo huo utapigwa kwenye uwanja wa Azam Complex majira ya saa 1:00 jioni. Azam FC na Stand United zinashuka dimbani kufungua raundi ya 12 ya ligi kuu ambapo mechi zingine zitachezwa kesho na Jumapili.
Azam FC kwasasa ina alama 23 sawa na Simba yenye alama 23 zikitofautiana idadi ya mbao ya kufunga na kufungwa. Endapo Azam FC itashinda leo itafikisha alama 26 na kuongoza ligi huku ikisubiri matokeo ya mechi ya kesho kati ya Ndanda FC na Simba.
Baada ya mchezo wa leo mabingwa hao watetezi wa Kombe la Mapinduzi watasafiri kuelekea Visiwani Zanzibar kwaajili ya michuano ya kombe hilo inayotarajiwa kuanza Januari mwakani. Azam FC ilitwaa kombe hilo Januari mwaka huu kwa kuifunga Simba kwenye mchezo wa fainali.
No comments:
Post a Comment