Friday, December 29, 2017

Bashe ashauri Serikali ikubali kukosolewa


Baada ya kuwaonya viongozi wa dini wasijihusishe na masuala yaliyo nje na usajili wao, mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe ameshauri Serikali ikubali kukosolewa.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana Alhamisi Desemba 28, 2017, katibu mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Projest Rwegasira alionya kuwa Serikali inaweza kufuta usajili wa taasisi zinazokiuka sheria ya usajili wao iwapo viongozi wa dini watajihusisha na masuala tofauti na masharti ya usajili wao.

Alitoa onyo hilo baada ya viongozi wa kidini kutumia ibada za sikukuu ya Krismasi kukosoa uendeshaji wa nchi, kutaka utawala wa sheria uheshimiwe na kuhoji sababu za kuzuiwa kuzungumzia siasa.

Lakini tamko la Serikali limekosolewa na wadau, akiwemo Bashe, ambaye aliandika maoni yake katika ukurasa wa Mwananchi ulioandika taarifa ya onyo hilo.

“Kesho tutazitaka taasisi za dini zihamasishe amani, maendeleo, zipongeze ‘Its important’ (ni muhimu) kukubali kukosolewa,” ameandika Bashe katika akaunti ya Twitter.

“Gvt should not do this as far as (Serikali haipaswi kufanya hivyo kwa kuwa) hazivunji sheria. Taasisi za dini zina haki kutoa maoni yao juu ya siasa, uchumi na masuala yote ya kijamii, viongozi wa dini wana nafasi yao.”

Mwingine aliyetoa maoni ni Mathias Mushi aliyesema: ‘’Nimewaza kwa sauti kama awamu hii inathubutu kutaka kuzifuta taasisi za kidini kwa kile wanachodai kukiuka miiko na maudhui ya taasisi zao jipe adhabu wewe unayekosoa, jipe adhabu wewe unayetofautiana nao, jipe adhabu wewe usiye mnafiki na msemakweli. Je, huu nao unaacha alama.”

Mchangiaji mwingine, Abedi Michael amesema: "Hiyo sheria inafanya kazi pale tu ambapo Serikali inakosolewa? Kwa nini viongozi hutumia dini kufanya mambo ya kisiasa? Nadhani ni wakati mwafaka wa kuirekebisha hiyo sheria ili kuwapa uhuru wa kuzungumza watumishi wa Mungu aliye hai.”

Mwananchi. 



No comments:

Post a Comment